NA EMMANUEL MBATILO, DAR ES SALAAM
WADAU wa Tapo kupitia uchambuzi wao wametaka kwenye Dira ya 2050 masuala ya Kijinsia yaweze kukondoishwa yote kuanzia kwenye malengo kwa kila kipaumbele masuala ya kijinsia yaingie.
Wito huo umetolewa leo Julai 12,2024 katika Kongamano la Kitaifa la Wanawake kuhusu ukusanyaji wa Maoni ya Dira ya Maendeleo ya Taifa 2050 lililofanyika katika Viwanja Vya TGNP-Mtandao Mabibo Jijini Dar es Salaam.
Akizungumza katika Kongamano hilo, Mwenyekiti wa Bodi-TGNP, Gemma Akilimali amesema wanatazamia sekta zote zijikite kwenye mchakato utakaobainisha masuala ya kijinsia katika mpango wa bajeti pamoja na utekelezaji.
“Kwa maandishi tunaweza kukuta suala la jinsia limetajwa kama kipengele, ukweli ni lazima masuala ya kijinsia yakondoishwe katika kila hatua, hii inaamanisha kufanya uchambuzi wa kina ya masuala yao ikiongozwa na takwimu sahihi zinazokidhi mipango na ugawaji rasilimali”. Amesema Gemma
Kwa upande wake Mkurugenzi Mtendaji wa TGNP- Lilian Liundi amesema takribani mashirika 200 yanayotetea masuala washiriki wa kongamano hilo kupitia mapendekezo yao ya Dira 2050.
Amesema washiriki wa kongamano hilo kupitia mapendekezo yao, watakwenda kuwaelimisha wanawake wengine ili kuongeza ushiriki mpana wa wanawake pamoja na kuelewa ni vipaumbele gani kwa pamoja tunataka viingie kwenye Dira 2050 katika kuandaa na kutekeleza.
Nae Mtaalamu wa Timu Kuu ya Uandishi wa Dira 2050, Amina Msengwa amesema wanaendelea kusisitiza wanawake washiriki kikamilifu kwani mpaka sasa tunaona wanawake ni wachache wanaoshiriki katika kutoa maoni.
Amesema wadau wa Tapo wameweza kuchambua vizuri Dira 2025 na chambuzi zake hasa katika upande wa kijinsia na kinachoonekana wanawake hao wanatamani kuona Dira 2050 ikihusisha mambo ya kijinsia hasa katika sehemu kubwa ya kiuchumi.
Mkurugenzi wa Mfuko wa Wanawake, Rose Marandu amesema katika uchambuzi wameona maeneo mengi ambayo tumefanikiwa ikiwemo kwenye elimu na kupeleka miundombinu ya nishati na maji kwenye maeneo ambayo yalikuwa na changamoto.
Amesema wanaweza kuleta madai mbalimbali ambayo ni maoni yao kwa ujumla ambapo wanataka yaingie kwenye Dira 2050 na mojawapo ni kusema Utu wa Mwanamke uweze kuheshimiwa na kila mtu kwenye Taifa hili.
“Mwanamke aonekane kiumbe ambaye ni mkamilifu wa taifa hili, mtu ambaye anamahitaji yake, aweze kushiriki kikamilifu kwenye ngazi mbalimbali za maendeleo yake binafsi pamoja na taifa kwa ujumla.
Pamoja na hayo amesema wanataka kuona taifa ambalo linakuwa kiuchumi na unamfikia mtu mmoja mmoja wa taifa hili, wanawake na vijana wa pembezoni.
Mwenyekiti wa Bodi-TGNP, Gemma Akilimali akizungumza katika Kongamano la Kitaifa la Wanawake kuhusu ukusanyaji wa Maoni ya Dira ya Maendeleo ya Taifa 2050 lililofanyika katika Viwanja Vya TGNP-Mtandao Mabibo leo Julai 12, 2024 Jijini Dar es Salaam.
Mkurugenzi Mtendaji wa TGNP- Lilian Liundi akizungumza katika Kongamano la Kitaifa la Wanawake kuhusu ukusanyaji wa Maoni ya Dira ya Maendeleo ya Taifa 2050 lililofanyika katika Viwanja Vya TGNP-Mtandao Mabibo leo Julai 12, 2024 Jijini Dar es Salaam.
Wadau wa Tapo wakifuatilia Kongamano la Kitaifa la Wanawake kuhusu ukusanyaji wa Maoni ya Dira ya Maendeleo ya Taifa 2050 lililofanyika katika Viwanja Vya TGNP-Mtandao Mabibo leo Julai 12, 2024 Jijini Dar es Salaam.