Na Wizara ya Madini.
Sekta ya Madini ni moja ya sekta muhimu nchini Tanzania, yenye mchango mkubwa katika Pato la Taifa, ajira, na maendeleo ya kijamii. Miongoni mwa madini yanayopatikana nchini Tanzania ni pamoja na Madini ya Metali (Metals) kama vile Dhahabu (Gold), Shaba (Copper), Chuma (Iron), Fedha (Silver) Nikeli (Nickel); Madini ya Viwandani (Industrial minerals), kama vile Kinywe (Graphite) Jasi (Gypsum)
Madini mengine ni Madini ya Nishati (Energy Minerals) kama vile, Makaa ya mawe (Coal),Urani (Uranium); Madini ya Vito (Gemstones) kama vile Almasi (Diamond) Ruby, Zamaradi (Emerald) na Madini ya kipekee ya Tanzanite yasiyopatikana popote ulimwenguni isipokuwa Tanzania; Madini Adimu (Rare earth elements) kama vile Neodymium, Lanthanum, Cerium; na Madini ya Ujenzi kama vile kokoto, mchanga, marble, chokaa.
Hivyo, Serikali imekuwa ikiweka mikakati mbalimbali ili kuhakikisha kwamba rasilimali hizi zinazopatikana kwa wingi hapa nchini zinanufaisha taifa na wananchi wake kwa ujumla.
Mchango wa Sekta ya Madini katika Pato la Taifa
Kwa mujibu wa ripoti ya Mwaka wa Fedha 2023/2024 iliyotolewa na Wizara ya Madini, sekta ya madini imechangia takribani asilimia 9.1 ya pato la taifa (GDP) ya Tanzania kufikia Mwaka 2022. Katika Mwaka wa Fedha wa 2023/2024, mchango wa sekta ya madini ulifikia shilingi trilioni 6.4, ukionyesha ukuaji wa kasi kutokana na mikakati iliyowekwa na serikali ya kuimarisha ukusanyaji wa mapato na kuboresha mazingira ya uwekezaji .
Ajira katika Sekta ya Madini
Ajira ni moja ya maeneo muhimu ambapo sekta ya madini imeleta mapinduzi makubwa. Hadi kufikia mwezi Machi 2024, sekta ya madini ilikuwa imezalisha ajira takribani 19,356, ambapo asilimia 97 ya ajira hizi zilikuwa zimeenda kwa Watanzania. Hii ni sawa na ajira 18,853 kwa Watanzania na ajira 505 kwa wageni. Serikali imeweka sheria na kanuni ambazo zinawapa kipaumbele Watanzania katika nafasi za ajira zinazotokana na uchimbaji wa madini, kuhakikisha kuwa wananchi wanapata fursa za ajira na kujipatia kipato.
Uwekezaji na Uchumi wa Madini
Uwekezaji katika sekta ya madini umeendelea kukua kwa kasi, huku Serikali ikihamasisha Kampuni za ndani na nje ya nchi kuwekeza katika utafiti, uchimbaji na uongezaji thamani madini. Kwa mwaka 2023, Kampuni za Kitanzania ziliuza bidhaa na huduma zenye thamani ya dola za Marekani bilioni 1.48 (Zaidi ya Tsh trilioni 3.75) migodini, ambayo ni sawa na asilimia 90 ya mauzo yote yaliyofanyika migodini. Hii inaonyesha umuhimu wa sekta binafsi katika kukuza sekta ya madini na uchumi kwa ujumla.
Mikakati ya Serikali
Kutokana na umuhimu wa sekta hiyo, Serikali ya Tanzania imeweka mikakati mbalimbali ili kuboresha sekta ya madini ili kuongeza tija Zaidi na kuikuza pia, kupitia Vision 2030: Madini ni Maisha na Utajiri, Serikali imepanga kufanya utafiti wa kina wa jiosayansi (High-Resolution Airborne Geophysical Survey) kwa angalau asilimia 50 kutoka asilimia 16 za sasa kwa nchi nzima kufikia mwaka 2030, utafiti huo unalenga kubaini maeneo mapya yenye madini yote yakiwemo haya ya muhimu na kuhamasisha uwekezaji zaidi katika eneo hilo. Mikakati mengine ni pamoja na:
1. Kuboresha Miundombinu: Serikali imewekeza katika kuboresha miundombinu ya barabara na umeme katika maeneo yenye migodi ili kurahisisha upatikanaji wa huduma muhimu na kuvutia uwekezaji.
2. Kutoa Mafunzo kwa Wachimbaji Wadogo: Serikali kwa kushirikiana na taasisi za elimu na mafunzo imeanzisha programu za mafunzo kwa wachimbaji wadogo ili kuwawezesha kutumia teknolojia bora na kuboresha uzalishaji.
3. Kuhamasisha Uongezaji Thamani: Serikali inahamasisha kampuni kuanzisha viwanda vya uongezaji thamani madini ndani ya nchi, badala ya kuuza madini ghafi nje ya nchi. Hii ni pamoja na uzalishaji wa bidhaa kama vile vito vilivyosafishwa, na bidhaa nyingine za thamani.
4. Usaidizi wa teknolojia kwa Uchimbaji Mdogo: Serikali kupitia Shirika la Madini la Taifa (STAMICO) imefanikiwa kununua mashine tano za uchorongaji kwa ajili ya kusaidia Wachimbaji Wadogo na kuwaokolea muda na gharama za uzalishaji. Mashine zingine 10 zinatajiwa kuwasili nchini hivi karibuni na kufikisha jumla ya mashine 15.
5. Utatuzi wa Changamoto ya Mitaji kwa Wachimbaji Wadogo: Serikali Kuptitia Wizara ya Madini na STAMICO imechukua hatua za kuwawezesha wachimbaji wadogo kupata mikopo na mitaji kwa kushirikiana na taasisi za fedha. Benki za CRDB, KCB, na NMB tayari zimeanza kutoa mikopo kwa riba nafuu kwa Wachimbaji hao na hivyo kuweza kununua vifaa vya kisasa na kuendesha shughuli zao kwa ufanisi zaidi. Katika kipindi cha Julai 2023 hadi Machi 2024, jumla ya shilingi bilioni 187 zilikopeshwa kwa wachimbaji wadogo.
Mifano ya Mafanikio
1. Mgodi wa Dhahabu wa Buckreef: Mgodi huo uliopo mkoani Geita unaomilikiwa kwa ubia kati ya STAMICO na Kampuni ya TANZAM2000, umeonesha mafanikio makubwa kwa kuzalisha wakia 13,577.43 za dhahabu katika kipindi cha Julai 2023 hadi Machi 2024, na kuchangia dola za Marekani 1,943,180.94 kama mrabaha, ada ya ukaguzi na ushuru .
2. Miradi ya Uwekezaji kwa Kijamii (CSR): Kampuni mbalimbali za madini hapa nchini zimewekeza kiasi cha shilingi 17,084,055,359.58 katika miradi ya maendeleo kwa jamii zinazozunguka migodi yao, ikiwemo ujenzi wa shule, hospitali, barabara na miundombinu ya maji.
Mustakabali wa Sekta ya Madini
Sekta ya madini nchini Tanzania ina mustakabali mzuri kutokana na mikakati iliyowekwa na Serikali kwa kushirikiana na wadau pamoja na uwekezaji unaoendelea kufanyika. Baadhi ya maeneo ambayo yanaonesha fursa kubwa ni pamoja na Madini Mkakati na Madini Muhumu kama vile lithium, nickel, kinywe na cobalt, ambayo ni muhimu katika uzalishaji wa betri za magari ya umeme na vifaa vingine vya kisasa vya teknolojia.
Hitimisho
Kwa ujumla, sekta ya madini nchini Tanzania imekuwa na mchango mkubwa katika maendeleo ya kiuchumi na kijamii. Mafanikio yaliyopatikana katika miaka ya hivi karibuni yanaonesha uwezo mkubwa wa sekta hii katika kukuza pato la taifa, kutoa ajira, na kuboresha maisha ya wananchi. Hata hivyo, Serikali kupitia Wizara ya Madini imeendelea kuweka mikakati endelevu na kuendeleza ushirikiano na sekta binafsi, na wadau wengine. Mikakati hiyo, itaiwezesha Tanzania kuendelea kunufaika zaidi na rasilimali zake za madini na kuhakikisha maendeleo endelevu kwa vizazi vijavyo.