Mkuu wa Mkoa wa Simiyu Mhe.Kenan Laban Kihongosi amewataka Maafisa Utumishi wa Halmashauri Mkoani Simiyu kuwatendea haki Walimu wanapofika katika Ofisi zao kutafuta huduma ili kuondoa malalamiko.
Ametoa rai hiyo alipokutana na kuzungumza na Walimu wa Shule za Msingi na Sekondari za Mkoa wa Simiyu katika ukumbi wa Shule ya Sekondari Kusekwa iliyoko Halmashauri ya Mji wa Bariadi.
Awali baadhi ya Walimu wa Halmashauri ya Mji wa Bariadi kikaoni hapo walieleza kutoridhishwa na utoaji wa huduma katika Ofisi ya Mkurugenzi Mtendaji Halmashauri ya Mji wa Bariadi.
Kufuatia changamoto hiyo Mkuu wa Mkoa wa Simiyu Mhe.Kenan Kihongosi akatoa rai kwa Maafisa Utumishi wa Halmashauri Mkoani humo kuhakikisha kuwa wanawatendea haki Watumishi kwa kutatua changamoto mbalimbali zinazowakabili Watumishi hao kwa upendo.
Amewataka Maafisa Utumishi kuondoa urasimu na kuacha majungu na badala yake kufanya kazi kwa bidii kwa kuzingatia Sheria kanuni na taratibu za Utumishi wa Umma ili kutimiza malengo mahsusi ya Serikali ya utoaji wa huduma bora kwa Wananchi.
Amewataka Maafisa Utumishi kuacha urasimu na badala yake wabadili mienendo Ili waweze kuwatendea vyema Watumishi ikiwa ni pamoja na kuzingatia Stahiki zao ili kiondoa malalamiko ya Watumishi.
Katika hatua nyingine Mkuu wa Mkoa Kihongosi ameagiza Uongozi wa Halmashauri kuhakikisha kunakuwepo msawazo sawa wa Watumishi wa Umma hususani Walimu kati ya maeneo ya mijini na Vijijini.
Ameagiza pia uongozi Wilayani Bariadi kusimamia suala la Stahiki za Wastaafu kwa wakati ili Watumishi hao waweze kupata haki yao mara baada ya kulitumikia Taifa kwa muda mrefu.
Mkuu wa Mkoa Kihongosi anakutana na Walimu na kuwasikiliza ikiwa ni utaratibu aliojiwekea kukutana na kuzungumza na Makundi mbalimbali ya Wananchi .
SIMIYU RS
02 Julai 2024.