Breaking

Saturday, 27 July 2024

RAIS SAMIA ASISITIZA UMUHIMU WA UHURU WA HABARI

 


* Amuagiza Waziri wa Habari, Mawasiliano na Teknolojia ya Habari Jerry Silaa kusimamia utekelezaji wa R4

* Awakumbusha wanahabari kuwa hakuna uhuru usio na mipaka


Julai 27, 2024

Mwandishi Wetu -Dar es Salaam

Rais Samia Suluhu Hassan amesisitiza umuhimu wa uhuru wa habari na kuvitaka vyombo vya habari nchini vizingatie mipaka ya uhuru huo.

Rais Samia alitoa kauli hiyo jana Ikulu, Dar es Salaam, baada ya kumuapisha Waziri wa Habari, Mawasiliano na Teknolojia ya Habari, Jerry Silaa.

"Wizara ya Habari ni muhimu sana katika utekelezaji wa ile falsafa yetu ya R4. Na hapa nitagusia uhuru wa habari kwamba lazima uendelee kusimamiwa kikamilifu," alisema.

Hata hivyo, Rais Samia alisisitiza kuwa "hakuna uhuru usiokuwa na mipaka yake. Kwa hiyo uhuru wa habari with (pamoja na) mipaka ya uhuru huo."

Rais Samia amemuagiza Silaa ashirikiane na wadau wa sekta ya habari katika majukumu yake mapya.

"Watu wa sekta ya habari ni muhimu sana, sana, sana kwa taifa hili. Vyombo vyote vya habari ni muhimu sana kwa taifa letu," alisisitiza.

Kauli ya Rais Samia inakuja huku Tanzania ikiwa imeshika nafasi ya kwanza katika nchi zinazolinda uhuru wa vyombo vya habari kwenye Jumuiya ya Afrika Mashariki (EAC) kwa mwaka 2024.

Hii ni kwa mujibu wa ripoti mpya ya mwaka huu ya taasisi ya kimataifa ya Reporters Without Borders (RSF).

Ripoti hiyo inaonesha kuwa Tanzania imepanda kutoka nafasi ya 143 kwa mwaka 2023 hadi nafasi ya 97 mwaka huu.

Kupanda huko kwa nafasi 46 ndani ya mwaka mmoja kunatokana na mafanikio makubwa ya kuimarika kwa mazingira ya uhuru wa vyombo vya habari nchini Tanzania kulinganisha na nchi zote za Afrika chini ya uongozi wa Rais Samia.

Kwa kushika nafasi ya 97 kati ya nchi 180 duniani, Tanzania imekuwa kinara wa nchi zote za Afrika Mashariki kwa uhuru wa habari mwaka huu.

Tanzania iko vizuri kwenye uhuru wa habari kuliko Kenya (102), Burundi (108), Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo (123), Uganda (128), Sudani Kusini (136), Rwanda (144) na Somalia (145).

Utafiti wa RSF umeangalia masuala kadhaa muhimu, ikiwemo misingi ya kisheria, hali ya kiuchumi, hali ya kisiasa, usalama wa wanahabari na dhana ya kijamii na kitamaduni.

Tangu alipoingia madarakani Machi 2021, Rais Samia ameimarisha uhuru wa vyombo vya habari nchini kama sehemu ya falsafa yake ya R4.

Falsafa ya R4 ya Rais Samia inazingatia maeneo ya Reform (mageuzi), Reconciliation (maridhiano), Resilience (ustahamilivu) na Rebuilding of the nation (kujenga upya).

Serikali ya Raia Samia imefungulia magazeti yaliyokuwa yamefungiwa na kuimarisha mazingira ya waandishi wa habari na vyombo vya habari kufanya kazi zao nchini.

Tangu Rais Samia alipoingia madarakani, matukio ya vyombo vya habari kufungiwa, kupigwa faini, waandishi kukamatwa au kuuwawa wakiwa katika majukumu yao ya kazi yametoweka nchini.

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia langolahabari@gmail.com au WhatsaApp: +255 621 896 990

Pages