Breaking

Sunday, 21 July 2024

MIZENGO PINDA ATAKA WANA CCM KUJIEPUSHA NA MANENO YA UCHOCHEZI

Na Munir Shemweta, MLELE

Waziri Mkuu Mstaafu ambaye ni Mjumbe wa Kamati Kuu ya Chama cha Mapinduzi Taifa Mhe. Mizengo Pinda amewataka wanachama CCM wanaotaka kugombea nafasi yoyote kujiepusha na maneno ya uchochezi yanayoweza kuharibu mahusiano baina yao.

Pinda amesema hayo tarehe 20 Julai 2024 wakati akizungumza na viongozi mbalimbali wa CCM wakiwemo madiwani, viongozi wa kata pamoja na wazee katika halmashauri ya Mpimbwe wilaya ya Mlele mkoa wa Katavi.

Amesema, kwa yoyote anayetaka kugombea nafasi ya uongozi ni vizuri akawa muangalifu na maneno ya uchochezi aliyoyaeleza kuwa, wakati mwingine yanaweza kumletea tabu wakati haipo.

"Chonde chonde sana usije ukaingia kwenye ugonjwa, unakaa unakuzungusha kicwa kwa sababu kuna mtu kaja kukuambia eeh kuma mtu fulani anakusema vibaya sasa hujathibitisha unaanza kutembea nayo na wewe usiende hivyo kwenye siasa hatuendi hivyo" amesema Mizengo Pinda

Amewataka wanapopelekewa maneno kuyapokea na kutulia huku wakijaribu kuyachunguza ili kuona ukweli au uongo kwa kile wanachoambiwa na kuweka wazi kuwa, wengi huponzwa na maneno ambapo amesisitiza, wana CCM kujaribu kupunguza maneno ya uchochezi yatakayosababisha kukwaruzana pasipo sababu ya msingi.

Kwa upande wake mbunge wa jimbo la Kavuu ambaye ni Naibu Waziri wa Ardhi Nyumba na Maendeleo ya Makazi Mhe. Geophrey Pinda ameeleza kuwa, hali ya kiasiasa ndani ya jimbo lake iko shwari na amekuwa akifanya vikao vya mara kwa mara kwa wananchi wa rika zote kupitia kata za jimbo hilo.

Hata hivyo, Mbunge huyo ameweka wazi kuwa, wakati mwingine kwa namna moja ama nyingine amashindwa kumfikia kila mwananchi kwenye jimbo hilo kutokana na idadi kubwa ya wakazi wake aliyoieleza kwamba imekuwa ikiongezeka siku hadi siku.

Amebainisha kuwa, kupitia wizara yake ya Ardhi Nyumba na Maendeleo ya Makazi wako mbioni kuweka mipango ya matumizi bora ya ardhi kwa kila kijiji ila wanachi wapate hati milki za ardhi na kuweza kuzitumia kwa matumizi mbalimbali ikiwemo kuchukulia mikopo benki.
Waziri Mkuu Mstaafu na Mjumbe wa Kamati Kuu ya Chama cha Mapinduzi Taifa Mhe. Mizengo Pinda akisalimiana na Mbunge wa jimbo la Kavuu katika halmashauri ya Mpimbwe mkoa wa Katavi Mhe. Geophrey Pinda alipokwenda kuzungumza na viongozi mbalimbali wa CCM jimboni humo tarehe 20 Julai 2024.
Waziri Mkuu Mstaafu na Mjumbe wa Kamati Kuu ya Chama cha Mapinduzi Taifa Mhe. Mizengo Pinda akizungumza kwenye mkutano wake na viongozi mbalimbali wakiwemo madiwani wa halmashauri ya Mpimbwe tarehe 20 Julai 2024 mkoani Katavi..
Sehemu ya washiriki wa mkutano wa Waziri Mkuu Mstaafu na Mjumbe wa Kamati Kuu ya Chama cha Mapinduzi Taifa Mhe. Mizengo Pinda katika halmashauri ya Mpimbwe mkoa wa Katavi tarehe 20 Julai 2024.
Mbunge wa Jimbo la Kavuu na Naibu Waziri wa Ardhi Nyumba na Maendeleo ya Makazi Mhe. Geophrey Pinda akiwa na baadhi ya wazee wa jimbo lake mara baada ya mkutano wao na Waziri Mkuu Mstaafu na Mjumbe wa Kamati Kuu ya Chama cha Mapinduzi Taifa tarehe 20 Julai 2024.
Mbunge wa Jimbo la Kavuu na Naibu Waziri wa Ardhi Nyumba na Maendeleo ya Makazi Mhe. Geophrey Pinda akizungumza wakati wa mkutano na Waziri Mkuu Mstaafu na Mjumbe wa Kamati Kuu ya Chama cha Mapinduzi Taifa tarehe 20 Julai 2024.

Waziri Mkuu Mstaafu na Mjumbe wa Kamati Kuu ya Chama cha Mapinduzi Taifa Mhe. Mizengo Pinda akiwa katika picha ya pamoja na wana CCM walioshiriki mkutano wake na viongozi mbalimbali wakiwemo madiwani wa halmashauri ya Mpimbwe tarehe 20 Julai 2024 mkoani Katavi.

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia langolahabari@gmail.com au WhatsaApp: +255 621 896 990

Pages