Breaking

Thursday 18 July 2024

MASELE : TAASISI ZA DINI ZINA WAJIBU MKUBWA WA KUSIMAMIA AMANI NA MSHIKAMANO KATIKA TAIFA

 

Makamu wa Rais mstaafu wa Bunge la Afrika (PAP) na mbunge mstaafu wa jimbo la Shinyanga mjini Mhe. Stephen Masele akishiriki Misa ya utolewaji wa Daraja la Upadre kwa mashemasi 11 iliyofanyika katika uwanja wa Kanisa la Mtakatifu Bikra Maria Mwombezi wa neema zote (Maria Mediatrix) Buhangija mjini Shinyanga

Makamu wa Rais mstaafu wa Bunge la Afrika (PAP) na mbunge mstaafu wa jimbo la Shinyanga mjini Mhe. Stephen Masele akisalimiana na Mapadre, Mashemasi, Watawa, Mafrateri na waamini kutoka sehemu mbalimbali za ndani na nje ya Jimbo la Shinyanga wakati wa Misa ya utolewaji wa Daraja la Upadre kwa mashemasi 11 iliyofanyika katika uwanja wa Kanisa la Mtakatifu Bikra Maria Mwombezi wa neema zote (Maria Mediatrix) Buhangija mjini Shinyanga
Makamu wa Rais mstaafu wa Bunge la Afrika (PAP) na mbunge mstaafu wa jimbo la Shinyanga mjini Mhe. Stephen Masele akitoa salamu wakati wa Misa ya utolewaji wa Daraja la Upadre kwa mashemasi 11 iliyofanyika katika uwanja wa Kanisa la Mtakatifu Bikra Maria Mwombezi wa neema zote (Maria Mediatrix) Buhangija mjini Shinyanga
Makamu wa Rais mstaafu wa Bunge la Afrika (PAP) na mbunge mstaafu wa jimbo la Shinyanga mjini Mhe. Stephen Masele akisalimiana na Askofu wa Jimbo la Shinyanga Mhashamu Liberatus Sangu (kushoto).
****
Makamwa Rais mstaafu wa Bunge la Afrika (PAP) na mbunge mstaafu wa jimbo la Shinyanga mjini mhe Stephen Masele amesema taasisi za dini nchini ikiwemo Kanisa Katoliki vina wajibu mkubwa wa kusimamia amani na mshikamano wa katika taifa.

Akitoa salamu leo Julai 18,2024 wakati wa Misa ya utolewaji wa Daraja la Upadre kwa mashemasi 11 iliyofanyika katika uwanja wa Kanisa la Mtakatifu Bikra Maria Mwombezi wa neema zote (Maria Mediatrix) Buhangija mjini Shinyanga Masele amesema “Taasisi za dini ikiwemo Kanisa katoliki lna wajibu mkubwa wa kujenga Imani kwa waumini wake, kutunza Amani na mshikamano wa taifa, lakini Pia taasisi za dini zinafanya kazi kubwa sana kuhamasisha amani, utulivu na mshikamano wa taifa, hebu fikiria taifa ama ulimwengu bila kuwa na taasisi za dini , bila kuwa na hofu ya Mungu Je tungeishi Vipi? Bila kuwa na imani ya dini na hofu ya Mungu dunia ingekuwa mahala pagumu sana pa kuishi".

"Hivyo nakupongeza sana baba Askofu Mhashamu Liberatus Sangu wewe binafsi kwa malezi bora unayotupatia, nawapongeza pia maparoko na mapadri wote kwa kuwalea vyema mapadri wapya hadi kufikia kupata daraja la upadri siku ya leo.

Binafsi nimefurahi sana kuungana nanyi kuwasherekea mapadri wetu wapya siku ya hii muhimu katika historia ya maisha yao",amesema Mhe. Masele. Masele ameongeza, "Uwepo wa mapadri 11 leo na mashemasi na mafrateri inaonesha kazi nzuri ya Kanisa katika kuwalea vyema vijana na kupenda kutumikia taifa la Mungu, hii inaonesha kuwa Kanisa letu lina 'future' Nawasihi Wazazi tuendelee kuwalea vijana wetu katika maadili mema ili tuweze kuwa na taifa lenye watu bora.

Mwisho nawatakia mafanikio mema katika majukumu yenu mapya mapadri wote wapya mliosimikwa leo katika daraja la upadri. Asanteni sana na Mungu awabariki wote",amesema. Kwa upande wa waumini wa Kikristo wa jimbo la Shinyanga mjini walionesha furaha na bashasha kubwa baada ya kumuona mbunge wao mstaafu mhe Stephen Masele akiwa ni miongoni mwao, walimshangilia Kila wakati alipokuwa akitoa hotuba yake, huku wengi wakionesha shauku kubwa ya kuzungumza naye na kupiga naye picha.

Mhe. Masele yupo mjini Shinyanga kwa shughuli za kifamilia .

Akiongea wakati wa shughuli hiyo mmoja ya waumini aliyejulikana kwa jina la Prisca Nkuba amesema,
“Kusema ukweli tume-miss sana mhe. Masele, ni mtu wa watu, mnyenyekevu na ni mtu mwenye kuheshimu watu wote bila kujali hali zao au madaraja yao kimaisha”. "Masele ni kiongozi makini na mwenye uwezo mkubwa sana , nadhani wananchi wamemkumbuka sana ndio maana wana furaha sana ya kumuona",ameongeza Muumini mwingine.

Kanisa Katoliki Jimbo la Shinyanga, limepata jumla ya Mapadre wapya 11 kwa wakati mmoja, kufuatia waliokuwa Mashemasi wa Jimbo kupewa Daraja la Upadre na Askofu wa Jimbo la Shinyanga Mhashamu Liberatus Sangu hii leo Julai 18,2024.

Misa ya utolewaji wa Daraja la Upadre imefanyika katika uwanja wa Kanisa la Mtakatifu Bikra Maria Mwombezi wa neema zote (Maria Mediatrix) Buhangija mjini Shinyanga, na imehudhuriwa na Mapadre, Mashemasi, Watawa, Mafrateri na waamini kutoka sehemu mbalimbali za ndani na nje ya Jimbo la Shinyanga.

Mapadre hao wapya ni Paschal Masunga wa Parokia ya Gula ambaye ametumwa kwenda kuwa Paroko msaidizi wa Parokia ya Lubaga mjini Shinyanga, Paschal Mahalagu wa Parokia ya Mwanangi ambaye ametumwa kwenda kuwa Paroko msaidizi wa Parokia ya Mtakatifu Luka-Bariadi mkoani Simiyu, Paschal Ntungulu wa Parokia ya Shishiyu ambaye ametumwa kwenda kuwa Paroko msaidizi wa Parokia ya Maganzo Wilayani Kishapu mkoani Shinyanga, Paschal Salyungu wa Parokia ya Mwamapalala ambaye ametumwa kwenda kuwa Paroko msaidizi wa Parokia ya Mwanangi wilayani Busega mkoani Simiyu na Peter Sayi wa Parokia ya Mtakatifu John-Bariadi ambaye ametumwa kwenda kuwa Paroko msaidizi wa Parokia ya Mhunze wilayani Kishapu mkoani Shinyanga.

Wengine ni Japhet Nyarobi wa Parokia ya Mtakatifu Luka-Bariadi ambaye ametumwa kwenda kuwa Paroko msaidizi wa Parokia ya Kitangili mjini Shinyanga, Philemon Nkuba wa Parokia ya Buhangija ambaye ametumwa kwenda kuwa Paroko msaidizi wa Parokia ya Mwanhuzi Wilayani Meatu mkoani Simiyu, Musa Majura wa Parokia ya Gula ambaye ametumwa kwenda kuwa Paroko Msaidizi wa Parokia ya Ndala mjini Shinyanga, James Chingila wa Parokia ya Mipa ambaye ametumwa kwenda kuwa Paroko msaidizi wa Parokia ya Kilulu Wilayani Bariadi mkoani Simiyu, James kija wa Parokia ya Chamugasa ambaye ametumwa kwenda kuwa Paroko msaidizi wa Parokia ya Mtakatifu John-Bariadi mkoani Simiyu na Osward Nkelege wa Parokia ya Bugisi ambaye ametumwa kwenda kuwa Paroko msaidizi wa Parokia ya Salawe iliyopo katika Halmashauri ya Wilaya ya Shinyanga (Vijijini).



Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia langolahabari@gmail.com au WhatsaApp: +255 621 896 990

Pages