Breaking

Saturday, 13 July 2024

DAWASA YAFUNGUA DIRISHA MAUNGANISHO HUDUMA YA MAJI UBUNGO, KINONDONI



Mamlaka ya Majisafi na Usafi wa Mazingira Dar es salaam (DAWASA) imezindua rasmi zoezi la utoaji wa vifaa vya maunganisho ya maji kwa wakazi waliokamilisha taratibu za maunganisho ya huduma ya Majisafi katika eneo lake la kihuduma katika Mkoa wa Dar es salaam na Pwani.

Akizungumza wakati wa kukabidhi vifaa vya maunganisho mapya katika Wilaya ya Kinondoni, katika kata za Goba na Wazo, Kaimu Afisa Mtendaji Mkuu DAWASA, Mhandisi Mkama Bwire ameeleza kuwa Mamlaka imejipanga kuhakikisha upatikanaji wa vifaa kwa ajili ya Maunganisho mapya yanapatikana.

"Tumekutana hapa kwa kazi moja ya kutekeleza agizo la Waziri wa Maji Mh.Jumaa Aweso (Mb) alipofanya ziara yake ya kikazi Mkoa wa Dar es salaam kuhakikisha wananchi waliolipia huduma ya Maji wanaunganishwa kwa wakati, na leo wananchi takribani 600 wa kata ya Goba na Wazo na leo tunakabidhi vifaa na kwenda kuungiwa huduma ya maji" ameeleza Mhandisi Bwire.

Mhandisi Bwire amewataka Wananchi ambao wameshapatiwa makisio ya gharama za maunganisho ya huduma walipie Ili waweze kupata huduma, na kusisitiza kadri wanavyowapatia wananchi huduma ni vyema walipie kulipa bili zao kwa wakati ili huduma iimarishwe.

Kwa upande wake, Katibu Itikadi na Uenezi wa Chama Tawala Mkoa wa Dar es salaam, ndugu Ally Bananga ameipongeza Serikali kupitia DAWASA kwa juhudi za kuhakikisha wananchi wanapata huduma ya maji huku akisisitiza wananchi kulinda na kutunza miundombinu ya maji ikiwa ni pamoja na kutoihujumu Mamlaka kwa kujiunganishia maji bila kufuata utaratibu.

Ndugu Gift Michael mkazi wa mtaa wa Salasala amepongeza juhudi za DAWASA kuwapatia huduma ya maji waliyoisubiri Kwa muda mrefu, huku akiweka wazi kuwa wananchi wa maeneo hayo watanufaika kiuchumi kufatia uwepo wa huduma ya maji.



Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia langolahabari@gmail.com au WhatsaApp: +255 621 896 990

Pages