Breaking

Tuesday 16 July 2024

"DAWASA ONGEZENI KASI KUWASIKILIZA NA KUTATUA KERO ZA WATEJA" - MHE MAKALLA



Katibu wa Itikadi, uenezi na mafunzo ya vijana wa Chama cha Mapinduzi (CCM) Taifa, Comrade Mhe. Amos Gabriel Makalla ameitaka Mamlaka ya Majisafi na Usafi wa Mazingira Dar es Salaam (DAWASA) kuimarisha huduma ya majisafi kwa wakazi wa Sinza wilayani Ubungo.

Ameyasema hayo wakati mwendelezo wa ziara yake katika Mkoa wa Dar es Salaam alipofanya mkutano wa hadhara katika viwanja vya TP Sinza ambapo amesisitiza uimarishaji wa huduma ya majisafi na salama kwasababu ni haki ya Mwananchi.

"Nawaagiza DAWASA mjitahidi kuweza kufanikisha utoaji wa huduma ya maji kwa wananchi hasa wa kata ya Sinza, hiyo ni haki yao kupata huduma ya maji na tusisubiri viongozi tufike na kutatua changamoto hiyo." ameeleza Mhe. Makalla

Hata hivyo ameipongeza Mamlaka kwa jitihada zinazoendelea kufanyika katika kwa utekelezaji wa mradi wa maji Sinza D ambao upo hatua ya mwishoni ya utekelezaji wake.

Naye Mkuu wa Wilaya ya Ubungo Mhe. Hassan Bomboko ameipongeza DAWASA kwa kuendelea kuboresha huduma ya maji kwa wananchi na kusisitiza wananchi kuwa wavumilivu katika kipindi hiki ambapo utekelezaji wa miradi ya maji inaenda kukamilika.

"Niwapongeze DAWASA kwa kazi kubwa mnayoifanya ya kuendelea kutatua changamoto ya wananchi kuhusu huduma ya maji ambayo ndio kero kubwa," ameeleza Mhe. Bomboko.

Nae Meneja wa DAWASA Magomeni, Julieth John ameahidi kutekeleza maagizo yaliyotolewa na Viongozi yanayolenga kuboresha huduma ya Majisafi katika Kata ya Sinza na maeneo mengine.





Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia langolahabari@gmail.com au WhatsaApp: +255 621 896 990

Pages