Breaking

Monday, 22 July 2024

BILIONI 16.5 KUKAMILISHA UJENZI WA CHUO KIKUU MZUMBE KAMPASI YA TANGA


Makamu Mkuu Chuo Kikuu Mzumbe, Prof. William Mwegoha (katikati) akiwasilisha  taarifa ya hatua za ujenzi wa Chuo Kikuu Mzumbe Kampasi ya Tanga kupitia mradi wa Elimu kwa Mageuzi ya Kiuchumi kwa Mkuu wa Mkoa wa Tanga, Mhe. Balozi Dkt. Batilda Salha Burian (kushoto) walipotembelea ofisini kwake. Kulia ni Naibu Makamu Mkuu wa Chuo - Mipango, Fedha wa Utawala, Prof. Allen Mushi
Mkuu Wa Mkoa Wa Tanga, Mhe. Balozi Dkt. Batilda Salha Burian (katikati) akizungumza na viongozi wa Chuo Kikuu Mzumbe mara baada ya kupokea taarifa ya hatua za ujenzi wa Chuo Kikuu Mzumbe Kampasi ya Tanga kupitia mradi wa Elimu kwa Mageuzi ya Kiuchumi.

Mkuu Wa Mkoa Wa Tanga, Mhe. Balozi Dkt. Batilda Salha Burian (katikati) akiwa kwenye picha ya pamoja na viongozi wa Chuo Kikuu Mzumbe mara baada ya kupokea taarifa ya hatua za ujenzi wa Chuo Kikuu Mzumbe Kampasi ya Tanga kupitia Mradi wa Elimu kwa Mageuzi ya Kiuchumi.


MKUU wa Mkoa wa Tanga, Mhe. Balozi Dkt. Batilda Salha Burian amesema kuwa Serikali ya Mkoa huo ipo tayari kuongeza nguvu ili kufanikisha ujenzi wa Chuo Kikuu Mzumbe Kampasi ya Tanga kupitia mradi wa Elimu ya Juu kwa Mageuzi ya kiuchumi.

Hayo yamesemwa leo Julai 22, 2024 ofisini kwake wakati akipokea taarifa ya utekelezaji wa mradi wa Ujenzi wa Chuo Kikuu Mzumbe ndaki ya Tanga kutoka kwa uongozi wa Chuo Kikuu Mzumbe uliofika ofisini hapo ukiongozwa na Makamu Mkuu wa Chuo hicho Prof. William Mwegoha.

Awali akizungumza wakati wa kukabidhi taarifa ya utekelezaji wa mradi huo Makamu Mkuu wa Chuo Kikuu Mzumbe, Prof. Mwegoha amesema mradi huo ni matokeo ya jitihada za Serikali katika kuimarisha elimu ya juu nchini.

"Chuo Kikuu Mzumbe ni miongoni mwa taasisi zinazonufaika na mradi huu ambao kwa sehemu kubwa umejikita katika kuboresha miundombinu ya kujifunza na kujifunzia. Sisi Chuo Kikuu Mzumbe tumepata nafasi ya kuanzisha Kampasi Jijini Tanga Wilaya ya Mkinga kata ya Gombero Kijiji cha Pangarawe. Alieleza Prof. Mwegoha.

Hatua za awali zimekwisha kukamilika kwa maana ya kupata eneo, kufanya tathmini ya athari kwa mazingira, kupata michoro sanifu ya majengo yanayotarajiwa kujengwa kutoka kwa mshauri elekezi, kutangaza zabuni ya kuanza ujenzi na sasa tupo kwenye hatua ya mwisho za ununuzi ili kazi iweze kukamilika wakati na ubora unaokusudiwa. Aliongeza Prof. Mwegoha.

Hata pamoja na jitihada na mafanikio hayo, Makamu Mkuu wa Chuo alieleza pia changamoto zinakabili utekelezaji wa miradi huo, ikiwa ni pamoja na kutokuwepo na miundombinu ya huduma za umeme, maji barabara kwenye endeo la ujenzi.

Akipokea taarifa hiyo Mkuu wa Mkoa wa Tanga, Mhe. Balozi Dkt. Batilda Burian amesema kuwa uwepo wa Chuo Kikuu cha Serikali Mkoani hapo ni fursa kwa wananchi na watumishi kujiongezea maarifa.

"Hatuna budi kuunga mkono juhudi hizi za serikali na Chuo na tutajitahidi kuendelea kushirikiana kutatua changamoto zilizopo tukiwahusisha wahusika kama TANESCO, TARURA na TANGAUWASA ili lengo la Serikali kupitia mradi huu liweze kutimia. Alisema Balozi Mhe. Dkt. Buriani.

Takribani Bilioni 16.5 zimetengwa kwa ajili ya ujenzi wa Jengo la Taaluma, Vyumba vya madarasa, Maktaba, Maabara ya Kompyuta, ukumbi wa mihadhara, zahanati na nyumba za watumishi zitakazojengwa katika eneo lenye ukubwa wa hekari 300.

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia langolahabari@gmail.com au WhatsaApp: +255 621 896 990

Pages