Breaking

Tuesday 16 July 2024

MAUNGANISHO HUDUMA MAJISAFI YASHIKA KASI DAR

Wateja mbalimbali wanaohudumiwa na Mamlaka ya Majisafi na Usafi wa Mazingira Dar es salaam (DAWASA) wameonyesha furaha yao baada ya kunganishwa na huduma ya maji na kuanza kupata huduma hiyo majumbani mwao.

Ndugu Kadrick Kipande mkazi wa Goba Mpakani ameshukuru DAWASA kwa kumfikia nyumbani kwake kwa haraka baada ya siku ya Jana kupatiwa vifaa vya maunganisho mapya na kumuungia huduma ya maji.

"Kwakweli sikutegemea kama ningepata maji kwa haraka kiasi hiki, siku Moja tu tangu nipigiwe simu kwenda kuchukua vifaa vyangu vya maunganisho na leo hii nimeungiwa huduma na napata maji nyumbani, niwapongeze DAWASA kwa kazi kubwa wanayofanya na kuwaomba waendelee na kasi hii sehemu zingine" ameeleza ndugu Kipande.

Ndugu Kipande ameongeza kuwa hapo awali ilimlazimu kutumia fedha nyingi kununua maji Tena yenye chumvi lakini sasa anaenda kuondokana na changamoto hiyo kwani anapata huduma ya Majisafi kutoka DAWASA.

Mhandisi Neema Mabike kutoka Mkoa wa kihuduma DAWASA Makongo ameeleza kuwa kazi kubwa inayoendelea kwasasa ni kuhakikisha wananchi wanaunganishiwa huduma ya maji kwa kasi ili kila mmoja aweze kufurahia huduma hiyo.

"Leo tupo katika maeneo mbalimbali tunayohudumia kuhakikisha wananchi waliopatiwa vifaa vya maunganisho ya majisafi wanaunganishwa na huduma hii, niwasihi wateja wote kua karibu na simu zao kwani mafundi wapo mitaani kuwafikia ili kufanikisha zoezi hili na hakuna mwananchi atakae rukwa bila kupata huduma" ameeleza Mhandisi Neema.

Mnamo tarehe 11/7/2024 DAWASA ili fungua rasmi pazia la ugawaji vifaa vya maunganisho ya majisafi kwa wateja walioomba na kulipia gharama zao za maunganisho, huku zoezi hilo likiwa ni endelevu.



Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia langolahabari@gmail.com au WhatsaApp: +255 621 896 990

Pages