Breaking

Saturday, 8 June 2024

WAZALISHAJI VYAKULA VYA MIFUGO WATAKIWA KUHAKIKI UBORA KWA MUJIBU WA SHERIA.

Na. Edward Kondela

Wazalishaij wa vyakula vya mifugo nchini wametakiwa kuwasilisha sampuli za vyakula hivyo katika Wakala ya Maabara ya Veterinari nchini (TVLA) kwa mujibu wa sheria ili kuhakiki ubora wa vyakula hivyo kabla ya kupelekwa sokoni.

Mtendaji Mkuu wa TVLA Dkt. Stella Bitanyi amebainisha hayo (08.06.2024) ofisini kwake jijini Dar es Salaam mara baada ya timu ya wataalamu kutoka Wizara ya Mifugo na Uvuvi na TVLA kukamilisha ukaguzi wa baadhi ya viwanda vya vyakula hivyo na kufanya kikao cha utoaji mafunzo kwa wazalisha, wauzaji na watumiaji wa vyakula vya mifugo kuhusiana na umuhimu wa uhakiki wa ubora wa vyakula vya Mifugo juni 6 Mkoani Arusha.

Dkt. Bitanyi ameongeza kuwa wazalishaji hao wanapaswa kuwasilisha sampuli katika maabara za wakala hiyo ili wapatiwe ushauri wa vyakula hivyo na sheria inataka chakula kisicho bora kisingizwe sokoni ili kumlinda mfugaji.

“Wazalishaji wa vyakula vya mifugo wahakikishe wanaendelea kuzalisha vyakula bora ili wafugaji waweze kukinunua chakula hicho, ili aweze kupata matokeo mazuri kwa mifugo yake.” Amesema Dkt. Bitanyi

Akiongoza timu ya ukaguzi, Mkurugenzi wa Huduma za Uchunguzi kutoka TVLA Dkt. Zacharia Makondo, amesema ni muhimu kwa vyakula vya mifugo kufika sokoni kama vilivyowekwa viwandani na kwamba wanaopuuza suala la kupima na kuhuisha usajili wa viwanda vyao watachukuliwa hatua za kisheria kwa mujibu wa Sheria ya Nyanda za Malisho na Rasilimali za Vyakula vya Wanyama.

Akizungumza jijini Arusha kwenye kikao cha utoaji mafunzo kwa baadhi ya wazalisha, wauzaji na watumiaji wa vyakula vya mifugo kuhusiana na umuhimu wa uhakiki wa ubora wa vyakula vya Mifugo Kanda ya Kaskazini inayojumuisha mikoa ya Arusha, Manyara na Kilimanjaro, Dkt. Makondo amefafanua kuwa katika ukaguzi wamegundua baadhi ya wauzaji wa vyakula vya mifugo kuchanganya vyakula wenyewe bila kufuata utaratibu.

Amesema ni makosa kwa wauzaji wa vyakula vya mifugo kuchanganya vyakula wenyewe na kuwauzia wafugaji na wauzaji wengine kufungua mifuko kutoka viwandani na kuchanganya na vyakula vingine.

Nao baadhi ya wadau walioshiriki katika zoezi la ukaguzi na kuhudhuria kikao hicho jijini Arusha wamepongeza kuwepo kwa ukaguzi wa vyakula vya mifugo ili kuhakikisha vinakuwa bora na kumnufaisha mfugaji ili apate matokeo mazuri ya mifugo yake.

Wakala ya Maabara ya Veterinari Tanzania (TVLA), inatarajia kuendelea kutoka elimu na kufanya ukaguzi wa rasilimali na vyakula vya mifugo katika kanda mbalimbali za wakala hiyo pamoja na kusimamia sheria ili wafugaji ili waweze kufuga kwa tija na kupata matokeo bora kupitia ufugaji.


Mtendaji Mkuu wa Wakala ya Maabara ya Veterinari nchini (TVLA), Dkt. Stella Bitanyi akizungumzia umuhimu wa wazalishaij wa vyakula vya mifugo nchini kutakiwa kuwasilisha sampuli za vyakula hivyo katika wakala hiyo kwa mujibu wa sheria ili kuhakiki ubora wa vyakula hivyo kabla ya kupelekwa sokoni juni 8, 2024 ofisini kwake jijini Dar es Salaam.
Mkurugenzi wa Huduma za Uchunguzi kutoka Wakala ya Maabara ya Veterinari Tanzania (TVLA) Dkt. Zacharia Makondo akifungua kikao cha mafunzo kwa wazalishaji, wauzaji na watumiaji wa vyakula vya mifugo kuhusiana na umuhimu wa uhakiki wa ubora wa vyakula vya Mifugo, sheria ya uendelezaji wa maeneo ya malisho na rasilimali za vyakula vya Mifugo pamoja na kufanya usajili wa Kampuni kwenye mfumo wa Wizara wa kutoa vibali wa MIMIS ili waweze kupata cheti cha kufanya biashara Juni 6, 2024 kwenye ukumbi wa Hazina ndogo Arusha.
Mtaalam wa Mifugo kutoka Idara ya Malisho na Rasilimali za vyakula vya Mifugo wa Wizara ya Mifugo na Uvuvi Bi. Theodata Sallema akiwasilisha mada kwa wazalishaji, wauzaji na watumiaji wa vyakula vya mifugo kuhusiana na umuhimu wa kusajili Kampuni kwenye mfumo wa Wizara wa kutoa vibali wa MIMIS ili waweze kupata cheti cha kufanya biashara pamoja na sheria ya uendelezaji wa maeneo ya malisho na rasilimali za vyakula vya Mifugo Juni 6, 2024 kwenye ukumbi wa Hazina ndogo jijini Arusha.
Meneja wa Wakala ya Maabara ya Veterinari Tanzania (TVLA) Kanda ya Kaskazini Arusha, Dkt. Rowenya Mushi akiwasilisha mada kwenye kikao cha mafunzo kwa wazalisha, wauzaji na watumiaji wa vyakula vya mifugo kuhusiana na umuhimu wa uhakiki wa ubora wa vyakula vya Mifugo Juni 6, 2024 kwenye ukumbi wa Hazina ndogo jijini Arusha.
Mkuu wa Kitengo cha Sayansi ya Wanyama wa  Wakala ya Maabara ya Veterinari Tanzania (TVLA) Dkt. Scholastika Dotto akiwasilisha mada kwenye kikao cha mafunzo kwa wazalisha, wauzaji na watumiaji wa vyakula vya mifugo kuhusiana aina mbalimbali za uhakiki wa ubora wa vyakula vya hivyo zinazofanya na TVLA Juni 6, 2024 kwenye ukumbi wa Hazina ndogo jijini Arusha.
Sehemu ya washiriki wa mafunzo kwa wazalishajk, wauzaji na watumiaji wa vyakula vya mifugo kuhusiana na umuhimu wa uhakiki wa ubora wa vyakula vya Mifugo, kufanya usajili wa Kampuni kwenye mfumo wa Wizara wa kutoa vibarli wa MIMIS ili waweze kupata cheti cha kufanya biashara pamoja na sheria ya uendelezaji wa maeneo ya malisho na rasilimali za vyakula vya Mifugo Juni 6, 2024 kwenye ukumbi wa Hazina ndogo jijini Arusha.
Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia langolahabari@gmail.com au WhatsaApp: +255 621 896 990

Pages