Breaking

Wednesday 19 June 2024

WATUMISHI WA UMMA WANAPASWA KUMUENZI MAREHEMU TIXON NZUNDA - DKT. MPANGO




Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Dkt. Philip Mpango amesema watumishi wa Umma wanapaswa kumuenzi aliyekuwa Katibu Tawala Mkoa wa Kilimanjaro marehemu Tixon Nzunda kwa kuwa waadilifu, wazalendo na kumtanguliza Mungu katika majukumu yao.

Makamu wa Rais amesema hayo wakati akizungumza na waombolezaji alipowasili nyumbani kwa aliyekuwa Katibu Tawala wa Mkoa wa Kilimanjaro Marehemu Tixon Nzunda, Moshi mkoani Kilimanjaro. Amesema marehemu Nzunda alikuwa kiongozi na mtumishi wa umma muadilifu na makini katika nafasi mbalimbali alizowahi kuzitumikia serikalini.

Amesema serikali imeguswa na msiba huo na inaungana na waombolezaji wote katika kipindi hiki kigumu. Aidha amewashukuru wananchi kwa kujitoa na kuwa pamoja na familia tangu ilipofikwa na msiba huo.

Vilevile Makamu wa Rais amewasihi watanzania kuendelea kuishi vema kazini, kuishi vema na marafiki pamoja na majirani. Amewaasa waombolezaji kupokea msiba huo kama ni mipango ya Mungu na kumuombea marehemu apumzike kwa amani.

Halikadhalika Makamu wa Rais ametoa salamu za rambirambi kwa familia ya marehemu Alphonce Edson aliyekuwa dereva wa Marehemu Tixon Nzunda waliofariki pamoja katika ajali ya gari Wilaya ya Hai mkoani Kilimanajro tarehe 18 Juni 2024.





Imetolewa na

Ofisi ya Makamu wa Rais

19 Juni 2024

Kilimanjaro.
Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia langolahabari@gmail.com au WhatsaApp: +255 621 896 990

Pages