Familia katika kaunti ya Kirinyaga nchini Kenya zina huzuni baada ya watu wawili kufariki na wengine wawili kupata majeraha mabaya baada ya lori walimokuwa wakisafiria kutumbukia mtoni.
Inasemekana kuwa lori hilo lilikuwa na watu watano kabla ya dereva kushindwa kulithibiti na kusababisha kuanguka kwenye Mto Nyamindi kwenye barabara ya Kiamutugu-Gituba huko Gichugu, kaunti ya Kirinyaga.
Kulingana na ripoti ya Citizen Digital, ajali hiyo ilisababisha vifo vya watu wawili, wawili kujeruhiwa vibaya na mtu mmoja kutangazwa kutoweka
Polisi katika eneo la tukio walithibitisha kuwa waathiriwa wanne waliokolewa na kusafirishwa haraka hadi Kituo cha Afya cha Kiamutugu, ambapo wawili kati yao walifariki kutokana na majeraha.
Polisi wameeleza kuwa wanamtafuta abiria ambaye ametoweka kufuatia ajali hiyo.
Source: Tuko News