NA EMMANUEL MBATILO, DAR ES SALAAM
WADAU wa Semina za Jinsia na Maendeleo wameelezea matarajio yao katika bajeti ya mwaka 2024/2025 ambapo wanatarajia uboreshwaji katika sekta maji, afya na elimu kutokana na kuonekana kuwa na changamoto kwenye maeneo mengi.
Akizungumza katika Semina za Jinsia na Maendeleo (GDSS) leo Juni 12, 2024 Jijini Dar es Salaam Mwanaharakati Bi.Nanteka Maufi amesema kuwa watarajia kuona maboresho makubwa katika Wizara ya Afya ambapo Serikali inatakiwa kuongeza vifaa tiba mahospitalini na kuachana na mtindo uliozoeleka kwa wanawake wajawazito kuombwa kutoa pesa kwaajili ya kujifungua wakati huohuo kutakiwa kununua baadhi ya vifaa kwa ajili ya huduma hiyo.
Amesema matibabu kwa wazee imekuwa ni changamoto kubwa licha ya kupewa kadi ya msamaha lakini bado kuna baadhi huduma za dawa wanaombwa kulipia ingawa hawana uwezo wa kufanya malipo hayo.
"Kwenye suala la wazee tulitamani sana huduma kwa wazee iwe bure, hata ikiwezekana suala la makazi wapate bure badala ya kuwapeleka Nunge kwenye vituo maalumu vya malezi, wajengewe makazi wao binafsi mfano Zanzibar wanasehemu salama ambazo wamejengewa". Amesema.
Kwa upande wake,Mwenyekiti wa Kituo cha Taarifa na Maarifa Kata ya Majohe Bi.Tabu Ally ameeleza mambo ambayo wanatamani yaboreshwe katika sekta ya elimu ambapo amesema ujenzi wa madarasa na kuongezwa kwa walimu hasa katika maeneo ya vijijini kutaongeza ufanisi.
"Tunatamani kwenye sekta ya elimu,walimu wapelekwe vijijini lakini kikubwa hasa wawe wanatafutwa walimu ambao wamesoma vijijini kwao, suala la kumtoa mwalimu Dar es salaam unampeleka Kibondo haileti maana kwasababu hata kule kuna walimu lakini bado serikali inapoteza mapato kumuhamisha mwalimu kumpleka sehemu nyingine" Bi.Tabu ameeleza.