SHIRIKA la Utafiti na Maendeleo ya Viwanda Tanzania (TIRDO) pamoja na Tume ya Tehama wamesaini makubaliano ya kuendeleza teknolojia katika kufikia Uchumi wa Kidigitali nchini.
Makubaliano hayo yamesainiwa katika ofisi za makao makuu ya TIRDO yaliopo Msasani jijini Dar Es Salaam.
Mkurugenzi Mkuu wa TIRDO Prof.Mkumbukwa Madundo Mtambo amesema kuwa wamefikia makubaliano hayo ya kuanzisha Maabara ya teknolojia ili kuhakikisha wataalam wanapata sehemu ya kupata ujuzi na kuandaa vifaa vya Tehama kwa ajili ya sekta mbali mbali nchini pamoja na Viwanda.
Kwa upande wake Mkurugenzi Mkuu wa Tume ya Teham Dr. Nkundwe Moses Mwasaga amemshukuru Mkurugenzi Mkuu wa TIRDO kwa kuwakubalia kuunganisha nguvu katika kuendeleza Tehama nchini Tanzania. ‘’TIRDO ni shirika kongwe nchini, mna wataalam wa kutosha , naamini kwa ushirikiano huu tunakwenda kutatua changamoto za Tehama nchini pamoja na kuzalisha wataalam wengi’’ aliongeza Dr.Mwasaga.
Mkurugenzi wa TEHAMA kutoka TIRDO Dr.Masoud Masoud amesema kuwa pamoja na ujenzi wa Maabara ya Kisasa ya Tehama lakini taasisi zote mbili zitashirikiana katika sekta zingine kama kuunganisha vifaa vya Kielektoniki(Assembly), kufanya matengezo vifaa vilivyoharibika, kutoa mafunzo ya kitaalam kwa wataalam wa ICT na kuhuisha vifaa vilivyokwisha muda wake (refabrication)
Shirika la Utafiti na Maendeleo ya Viwanda Tanzania (TIRDO) ni Shirika la utafiti na maendeleo ya taaluma mbalimbali lililoanzishwa kwa Sheria ya Bunge Na. 5 ya 1979 na ilianza kufanya kazi tarehe 1 Aprili, 1979.
Jukumu lake ni kusaidia sekta ya viwanda Tanzania kwa kutoa utaalam wa kiufundi na huduma za usaidizi ili kuboresha zao msingi wa teknolojia. Zaidi ya hayo, mamlaka ya TIRDO ni kufanya utafiti uliotumika kwa ajili ya maendeleo ya teknolojia zinazofaa, na kuongeza thamani kwa rasilimali asilia kupitia usindikaji wa viwanda.
TIRDO imejikita katika Kufanya na kuhimiza utekelezaji wa utafiti uliotumika ulioundwa kuwezesha tathmini, maendeleo na matumizi ya nyenzo za ndani katika michakato ya viwanda, Kufana Utafiti wa mbinu na teknolojia za viwanda vya ndani na nje ya nchi na kutathmini kufaa kwao kupitishwa na kutumika katika uzalishaji wa viwanda, Kukuza na kutoa vifaa kwa ajili ya mafunzo kwa wafanyakazi kwa ajili ya kutekeleza maombi utafiti wa kisayansi na viwanda, Kuendesha mfumo wa uhifadhi wa nyaraka ili kusambaza taarifa kuhusu utafiti uliotumika pamoja na Kutoa uwezo wa kiufundi ili kukabiliana na uchafuzi wa mazingira viwandani.