Breaking

Friday, 14 June 2024

TGNP, WADAU WA MAENDELEO WAICHAMBUA BAJETI YA SERIKALI


Na mwandishi wetu, Dar es Salaam

Mtandao wa Jinsia Tanzania (TGNP) kwa kutambua umuhimu wa ushiriki wa wananchi katika michakato ya bajeti na michakato ya maendeleo kwa ujumla umekuwa ukishirikiana na wadau mbalimbali katika kuhakikisha kwamba wananchi wanashiriki ipasavyo katika michakato hiyo pamoja na kutathimini mipango ya maendeleo ya taifa letu.

Hayo yamesemwa Ijumaa Juni 14, 2024 na Mkurugenzi Mtendaji wa TGNP, Lilian Liundi akiongea katika siku ya pili ya Jukwaa la Kijiwe cha Kahawa katika ukumbi wa mikutano wa ofisi za TGNP, Mabibo jijini Dar es Salaam ikiwa ni siku ya pili ya kijiwe hiko ambapo kiliangazia kufanya tathimini ya bajeti kuu ya serikali, mpango wa tatu wa maendeleo pamoja na Dira ya Taifa ya Maendeleo ambapo amebainisha kuwa wao TGNP na wadau wengine walishiriki katika utengenezaji wa Dira ya Taifa ya Maendeleo 2025 ambapo matunda na manufaa katika eneo la jinsia wana mchango wao.

Ameendelea kwa kusema kuwa, kila mwaka TGNP wamekuwa na utamaduni wa kutathimini mpango wa maendeleo wa mwaka ambao unaotokana na utekelezaji wa Dira ya Taifa ya Maendeleo.

Akizungumzia kuhusu Mpango wa Tatu wa Maendeleo wa Taifa wa mwaka 2023/2024 katika jicho la kijinsia, Bi. Liundi ameeleza kuwa, mpango huo ni wa mwisho wa kutekeleza Dira ya Taifa ya Maendeleo 2025, ambapo mipango yote iliyopita ilikuwa na malengo yanayofanana.

Ameyataja malengo hayo kuwa ni pamoja na kuwa na uchumi shindani, amani na utulivu, kuimarisha miundombinu ya uzalishaji na ufikiwaji wa nishati ya uhakika, kuimarisha mazingira wezeshi ya biashara na uwekezaji, kuboresha mifumo ya elimu, mafunzo pamoja na kufungamanisha tafiti, maendeleo ya kilimo na uzalishaji kiuchumi.

Kupitia malengo hayo hakusita kutoa maoni yake katika jicho la kijinsia ambapo amesema "Kwa mujibu wa Sensa ya Watu na Makazi imeonesha kuwa idadi ya wanawake nchini ni zaidi ya asilimia 51 ya wananchi wote, hivyo unapotaka kuwa na uchumi shindani ni lazima kundi hilo la wananchi washiriki kukikamilifu katika ujenzi wa uchumi huo".

"Tunapozungumzia nishati, mwanamke anaingia hapo, watu wenye ulemavu wanaingia hapo, unaposema wawekezaji wameongezeka je ongezeko hilo ni la wanawake? watu wenye ulemavu, vijana na idadi yao ni ngapi?"

Katika kufanikisha hilo, Liundi ameishauri serikali kutenga fungu la kutosha pamoja na rasilimali zote ambazo zitarahisisha na kuruhusu mchakato shirikishi wa makundi yote katika uandaaji wa dira ijayo (Dira ya Taifa ya Maendeleo 2050)

Vilevile ametoa rai kwa serikali kutoa takwimu zenye mchanganuo wa jinsi pindi wanapofanya tathimini ya wanufaika katika mpango huo ili jamii iweze kubaini ni kundi gani limenufaika katika utekelezaji wa mpango huo wa tatu wa maendeleo.

Akichangia mada katika jukwaa hilo, Kaimu Mkuu wa Idara ya Harakati na Ujenzi wa Nguvu za Pamoja kutoka TGNP, Flora Ndaba amesema, kuongezeka kwa bajeti ya kilimo kumeleta matokeo chanya ikiwemo kuwa na zaidi ya chakula kwa zaidi ya asilimia 120 jambo ambalo limeleta matokeo chanya kwenye kupambana na tatizo la udumavu ambapo kwa mujibu takwimu za Shirika la Umoja wa Mataifa la Kuhudumia Watoto (UNICEF) kutoka mwaka 1999 hadi 20226tatizo la udumavu kwa watoto wenye umri chini ya miaka mitano nchini limepungua kutoka asilimia 48.3 hadi kufikia asilimia 25.3.

Kwa upande wa elimu, Bi. Ndaba amesema, kwa sasa idadi ya wanafunzi wanaonza na kumaliza elimu ya msingi imeongezeka ambapo hadi kufikia mwaka 2023 ambapo kumeshuhudiwa ongezeko kubwa ikilinganishwa na miaka 15 iliyopita ambapo kulikuwa na asilimia 28 hadi kufikia asilimia 84.
Katika mchanganuo huo, asilimia 51 wanafunzi waliokuwa wanaanzishwa shule walikuwa ni wakiume huku asilimia 49 wakiwa ni wakike jambo ambalo limeonesha kuwepo kwa jitihada za kuhamasisha watoto wa kike kuingia shuleni.

Naye Afisa Programu Mwandamizi kutoka GNP, Anna Sangai ameiomba serikali kuijengea uwezo jamii kwa kutoa elimu ya kutosha juu ya Dira ya Taifa ya Maendeleo 2050 ili wawe na ufahamu wa kutosha wakati wa kutoa maoni lakini pia kuwa uzingatiaji mkubwa wakati wa kukusanya maoni ya dira hiyo kwa kuyafikia makundi yote ikiwemo kundi la watu wenye ulemavu ambao ni asilimia 2.3 ya idadi ya watu wote nchini.

Kwa upande wake Mtafiti Huru wa Masuala ya Sera katika upande wa rasilimali za maliasili Francis Mkasiwa, amesema miradi mingi ya maji inayotekelezwa hivi inapaswa kupelekewa fedha za kutosha na kwa wakati ili kuongeza kasi ya utekelezaji wake ambapo kwa kufanya hivyo itafanikisha kukamilika kwa miradi hiyo na hatimaye azma ya kumtua Mama Ndoo Kichwani itafanikiwa.

Tangu kuanzishwa kwa Mtandao wa Jinsia Tanzania (TGNP) imetumia mikakati ya kushawishi sera za kitaifa/ kisekta, mipango na michakato ya bajeti kwa kukabiliana na mahitaji ya wanawake na ya kimkakati mfano upatikanaji wa huduma za afya na maji.

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia langolahabari@gmail.com au WhatsaApp: +255 621 896 990

Pages