Breaking

Tuesday 25 June 2024

STAMICO YADHAMIRI KUWAWEZESHA WACHIMBAJI WADOGO WA MADINI



Shirika la Madini la Taifa (STAMICO) limeelezea Mipango yake ikiwemo kuendelea kuwawezesha Wachimbaji Wadogo wa Madini nchini, huku msisitizo ukiwekwa kwenye ununuzi wa mitambo na huduma za uchorongaji ili kuwasaidia kupata taarifa za miamba, hatimaye wachimbe kwa tija.

Hayo yalielezwa Juni 24, 2024 na Meneja Uwezeshaji Uchimbaji Mdogo kutoka STAMICO Bw. Tuna Bandoma kwenye Wiki ya Madini inayokwenda sambamba na Kongamano la Wachimba Madini, Mkutano wa Shirikisho la Vyama vya Wachimbaji wa Madini Tanzania (FEMATA) pamoja na maonesho ya madini na vifaa vya uchimbaji inayoendelea katika Ukumbi wa Mikutano wa Jakaya Kikwete Convention Center jijini Dodoma.

Aliongeza kwamba, mitambo hiyo itawahudumia zaidi wachimbaji wadogo wenye leseni hai huku akitaja huduma hiyo kutumia gharama ndogo ambazo itamhitaji mchimbaji kuchangia, ambazo ni nafuu ikilinganishwa na uhalisia wa gharama za uchorongaji.

Akizungumzia mgawanyo wa mitambo hiyo, Bandoma alisema ugawaji wake umezingatia maeneo yenye idadi kubwa ya shughuli za uchimbaji mdogo ikiwemo Mkoa wa Geita na uwepo wa miradi ya mashirika makubwa ili kusaidia kuhifadhi mitambo hiyo.

Vilevile, akizungumzia kuhusu uwezeshaji wa kifedha, Bandoma alisema STAMICO itaendelea kuimarisha taarifa za wachimbaji wadogo ili waweze kuaminika na kukopesheka na taasisi za fedha.

Naye, Muhasibu kutoka FEMATA Bw. Gregory Kibusi alitumia fursa hiyo kuipongeza STAMICO kwa kuendelea kuwa karibu na wachimbaji wadogo katika kuwawezesha kujiinua kiuchumi kupitia mitambo ya uchorongaji.

STAMICO imeendelea kutekeleza majukumu yake ya kuwasimamia na kuwaendeleza wachimbaji wadogo kwa kutoa elimu ya uchimbaji bora unaotumia teknolojia ya kisasa, kuandaa mikutano inayowakutanisha na wadau wa ndani na nje ya nchi pamoja na kuleta mitambo ya uchorongaji maalum kwao inayowasaidia kujua kiwango cha rasilimali katika maeneo yao ya uchimbaji.


Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia langolahabari@gmail.com au WhatsaApp: +255 621 896 990

Pages