Breaking

Saturday, 29 June 2024

SILLO AHITIMISHA ZOEZI LA MAFUNZO YA UPANDISHWAJI VYEO



Na Mwandishi wetu;-

Naibu Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi Mhe. Daniel Sillo (Mb), amehitimisha zoezi la Mafunzo ya upandishwaji vyeo ya Uongozi Mdogo kwa Cheo cha Sajini Meja (SM) na Sajini Taji (S/SGT) wa Polisi Kozi Na. 1/2023/2024 katika Chuo cha Maafisa wa Polisi Tanzania kilichopo Kidatu Mkoani Morogoro.

Akihutubia katika hafla hiyo Juni 28, 2024 Mhe. Sillo amesema kuwa, anatambua mafunzo yalikuwa ya muda mfupi lakini yenye mambo mengi muhimu yaliyofundishwa kwa njia ya nadharia na vitendo na mada zote zilifundishwa.

"Lengo ni moja tu kwamba mtakaporejea kwenye vituo vyenu vya kazi muweze kuwa mmepata ujuzi na mbinu za uongozi za kuwasaidia katika usimamizi wa majukumu ya kazi mtakayopangiwa. Ni vyema nichukue fursa hii kuwapongeza wakufunzi wote waliowezesha kukamilika kwa mafunzo haya kwa ufanisi kama ninavyojionea hapa, amesema nimeelezwa na Mkuu wa Chuo kuwa wakati wote wa mafunzo mmeonesha kuwa wenye nidhamu ya hali ya juu na mmejitolea kwa moyo wa dhati katika kushiriki kwenye vipindi vyote vya mafunzo bila kutegea vipindi" Alisema Mhe. Sillo

Pia amewataka wale wote ambao bado wanaendelea na vitendo vya ukiukwaji wa maadili waache mara moja na wabadilike kifikra ili waweze kuwatendea haki wananchi kwani dhamana waliyopewa katika nchi hii ni kubwa na vyeo hivyo viwasaidie katika kuwasimamia Askari wa chini ili nidhamu na uadilifu viimarike Jeshini katika kuepuka malalamiko hayo.

Mhe. Sillo pia amewaelekeza kuhakikisha wanadhibiti ajali za barabarani, Biashara Haramu za Dawa za Kulevya ambayo inaathiri afya ya vijana pamoja na kushughulikia kesi za unyanyasaji wa kijinsia na ukatili wa Wanawake na Watoto vikiwemo vitendo vya ukatili dhidi ya makundi maalum wakiwemo watu wenye ulemavu wa Ngozi (Albino).

"Kama kuna jambo linaniumiza sana ni ajali za Barabarani hapa nitoe rai kwa wadau wote wa usafirishaji Madereva, Watumiaji wa Barabara na Jeshi la Polisi Kikosi cha Usalama Barabarani tushirikiane kusimamia Sheria na kuzingatia alama za Barabarani zilizowekwa kwa mujibu wa Sheria"

Aidha, amemshukuru Rais wa Jamhuri wa Muungano wa Tanzania Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan kwa kazi kubwa na iliyotukuka anayofanya katika kuhakikisha nchi inakuwa salama muda wote ikiwa ni pamoja na kuliwezesha Jeshi la Polisi kwa kuwapandisha vyeo Askari katika ngazi mbalimbali sambamba na kutoa kibali cha ajira kwa Askari wapya.

"Nizidi kutilia mkazo kwenye jitihada anazozifanya IGP Camillus Wambura za kupeleka Wakaguzi wa Polisi hadi ngazi ya Kata/Shehia kwa kutambua umuhimu wa Wakaguzi wa Kata/Shehia nchi nzima kwa kuwapa motisha na kuwawekea mazingira mazuri ya kazi kama ambavyo Mhe. Mhandisi Hamad Masauni Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi alivyokwisha anza kwa kuwatambua wanaofanya vizuri kila mwaka" Alisema

Awali katika taarifa yake Kamishna wa Polisi Operesheni na Mafunzo CP Awadhi Juma Haji aliishukuru Serikali ya Awamu ya Sita inayoongozwa na Rais Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan kupitia Wizara ya Mambo ya Ndani ya Nchi kwa jinsi wanavyoliwezesha Jeshi la Polisi kwa kulipatia Vitendea kazi vya kutosha pamoja na Rasilimaliwatu.

Mhe. Mgeni Rasmi Kozi hii unayokwenda kuihitimisha hii leo Chuoni hapa ni miongoni mwa Kozi zilizokuwa zikiendelea katika vyuo vyetu vingine hapa Nchi ambapo inafanya jumla Askari 3464 ambao wamedhuria Mafunzo na kuhitimu katika ngazi mbalimbali.
Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia langolahabari@gmail.com au WhatsaApp: +255 621 896 990

Pages