Breaking

Saturday, 29 June 2024

PINDA ATAKA MRADI UJENZI CHUO CHA ARDHI MOROGORO KUWEKEWA NGUVU

Na Munir Shemweta, MOROGORO

Naibu Waziri wa Ardhi Nyumba na Maendeleo ya Makazi Mhe. Geophrey Pinda ametaka mradi wa ujenzi wa Chuo cha Ardhi Morogoro unaojumuisha eneo mahali chuo kilipo na eneo la mlima Kola kuwekewa nguvu ili uweze kukamilika kabla ya muda uliopangwa.

Mhe. Pinda ametoa kauli hiyo leo tarehe 29 Juni 2024 wakati alipokwenda kukagua eneo la ujenzi wa mradi huo katika eneo la mlima Kola mkoani Morogoro.

Mradi wa ujenzi wa Chuo cha Ardhi Morogoro unaojumisha mahali chuo kilipo pamoja na eneo la Mlima Kola umeelezwa kuchukua miaka 20 mpaka kukamilika kwake mwaka 2043 na utagharimu kiasi cga shilingi bilioni 70 ambapo bilioni 64 zitawekezwa eneo la mlima Kola na bil 6 kwenye kampasi ya chuo Kilakala.

Mradi huo unajumuisha Jengo la Utawala, Madarasa, Maktaba, Hosteli za Wanafunzi, Kumbi kubwa za kufundishia, Zahanati, Migahawa pamoja na maeneo ya kuabudia.

Kwa mujibu wa Kaimu Mkuu wa Idara ya Taaluma Pius Kafefa, vyanzo vya mapato kwa ajili ya ujenzi wa mradi huo wa chuo cha ARIMO ni ada za wanafunzi, miradi mbalimbali ya chuo kama vile ushauri wa kitaaluma, fedha kutoka serikalini pamoja na maombi kutoka kwa wafadhili.

Naibu Waziri wa Ardhi Mhe. Pinda amesema, ni vyema mradi huo ukawekewa nguvu ili uende kwa haraka kwa kuwa kuchukua muda mrefu kutafifisha uharaka wa maendeleo ya chuo.

"Kujipa muda mrefu kukamilisha mradi wa chuo chenu hakuko sawa kabisa na sisi tunataka mradi uishe haraka ili tuwe na matokeo ya muda mfupi sambamba na waanzishaji mradi kuushuhudia". amesema Mhe. Pinda.

Ameutaka uongozi wa chuo cha ARIMO kuandika mapendekezo ya namna ya kukamilisha ujenzi wa mradi huo kwa haraka ili wizara ya Ardhi Nyumba na Maendeleo ya Makazi ione namna ya kusaidia ili uishe kabla ya muda wa miaka 20 uliopangwa.

Mwenyekiti wa Bodi ya Chuo cha Ardhi Morogoro Profesa Ernest Kahanga ameeleza kuwa, changamoto kubwa inayokikabili chuo ni upungufu wa walimu pamoja na miundombinu ambapo ameweka wazi kuwa, kama chuo hicho kingetatua changamoto hizo kingefanikiwa kudahili takriban wanafunzi 3000 na kukifanya chuo kusonga mbele kwa kasi na kuondokana na utegemezi.
Kaimu Mkuu wa Idara ya Taaluma Chuo cha Ardhi Morogoro Pius Kafefa akitoa maelezo kwa Naibu Waziri wa Ardhi Nyumba na Maendeleo ya Makazi Mhe. Geophrey Pinda (wa pili kulia) kuhusiana na Mpango Kabambe wa mradi wa Chuo cha Ardhi Morogoro katika eneo la Mlima Kola mkoani Morogoro alipofanya ziara katika eneo hilo tarehe 29 Juni 2024.
Naibu Waziri wa Ardhi Nyumba na Maendeleo ya Makazi Mhe. Geophrey Pinda akionesha moja ya jengo kupitia Mpango kabambe wa Mradi wa ujenzi wa Chuo cha Ardhi Morogoro kwenye eneo la Mlima Kola alipofanya ziara ya siku moja mkoani Morogoro tarehe 29 Juni 2024. Kushoto ni Mwenyekiti wa Bodi ya Chuo Profesa Ernest Kahanga.
Mkuu wa Chuo cha Ardhi Morogoro (ARIMO) Charles Saguda akimuonesha Naibu Waziri wa Ardhi Nyumba na Maendeleo ya Makazi Mhe. Geophrey Pinda moja ya majengo yaliyopo kwenye Mpango Kabambe wa Mradi wa ujenzi wa majengo ya Chuo yaliyopo eneo la mlima Kola mkoani Morogoro tarehe 29 Juni 2024.
Mkuu wa Chuo cha Ardhi Morogoro (ARIMO) Charles Saguda akifafanua jambo kwa Naibu Waziri wa Ardhi Nyumba na Maendeleo ya Makazi Mhe. Geophrey Pinda wakati akikagua moja ya ujenzi wa madarasa ya chuo cha ARIMO alipofanya ziara chuo hapo tarehe 29 Juni 2024.
Mkuu wa Chuo cha Ardhi Morogoro (ARIMO) Charles Saguda akimfafanulia jambo Naibu Waziri wa Ardhi Nyumba na Maendeleo ya Makazi Mhe. Geophrey Pinda sehemu ya majengo yaliyopo kwenye Mpango Kabambe wa mradi wa ujenzi wa mradi wa chuo katika enao la Mlima Kola mkoani Morogoro alipofanya ziara chuo hapo tarehe 29 Juni 2024. (PICHA ZOTE NA WIZARA YA ARDHI)
Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia langolahabari@gmail.com au WhatsaApp: +255 621 896 990

Pages