Mhe. Pinda ameelezwa na mkandarasi wa mradi huo Wakala wa Majengo Tanzania TBA kuwa, ujenzi wa mradi huo ungekuwa umekamilika kwa wakati lakini kutokana na kuchelewa kwa baadhi ya vifaa kwa ajili ya ukamilishaji ujenzi wa mradi huo wa maktaba kumesababisha mkanadarasi kushindwa kutekeleza kazi yake kwa wakati
.‘’Mhe. Waziri, kazi hii tungeweza kumaliza ndani ya siku sitini lakini changamoto kubwa ni material tumeshindwa kukamilisha kutokana na kuchelewa kufika kwa baadhi ya vifaa kwa wakati na hivyo kutufanya tushindwe kukamilisha kazi hii’’ alisema Meneja wa Wakala wa Majengo Tanzania (TBA) mkoa wa Tabora Mhandisi Ebenezer Ngure.
Akizungumza wakati wa kukagua mradi wa ujenzi wa Maktaba ya Chuo cha Ardhi Tabora tarehe 15 Juni 2024, Naibu Waziri wa Ardhi Nyumba na Maendeleo ya Makazi Mhe. Geophrey Pinda amemuagiza mkandarasi wa mradi huo kuandika ripoti inayoonesha mahitaji yote na kumfikia ifikapo jumatano ya tarehe 19, 2024 ili afanyie kazi changamoto zinazokwamisha ujenzi kutokamilika kwa wakati.
Awali Chuo cha Ardhi Tabora, kilimueleza Naibu Waziri Mhe. Pinda kuwa, kuna baadhi ya vifaa ambavyo Mkandarasi Mshauri ameomba vibadilishwe ambapo mzabuni aliombwa kwenda kuvichukua lakini hakufika jambo lililomshangaza mhe. Pinda.
Naibu Waziri wa Ardhi ameagiza ubadilishaji wa vifaa kutoka kwa mzabuni kufanywa haraka kufikia jumanne ya tarehe 18, 2024 kwa kuwa wenye shinda ni chuo hivyo hawapaswi kusubiri mzabuni na badala yake chuo kifuatilie ili ujenzi wa jengo hilo ukamilike.
‘’Nilidhani hawa ndiyo wenye makosa lakini wenye makosa ni sisi, maelekezo yangu kufikia jumanne nne vifaa hivi vilivyozidi na kumpa mrejesho wa hatua mliyofikia’’ alisema mhe. Pinda
Meneja wa TBA alimhakikishia Mhe, Naibu Waziri wa Ardhi kuwa ndani ya miezi miwili baada ya kupatiwa vifaa watakuwa wamekamilisha ujenzi wa mradi huo wa Maktaba ya Chuo cha Ardhi na watafanya kazi hiyo kwa weledi mkubwa,
Mradi wa ujenzi wa Maktaba ya Chuo cha Ardhi Tabora ulianza tarehe 15/07/2014 ukitekelezwa chini ya Kampuni ya M/S Co Ltd kwa mkataba uliosaniwa na Wizara ya Ardhi Nyumba na Maendeleo ya Makazi ukiwa na thamani ya TSH 2,026,538,726.00 ambapo muda wa mkataba ulikuwa kipindi cha majuma 44 hivyo kutarajiwa kukamilika tarehe 18/05/2024.
Hata hivyo, kutokana na changamoto kadhaa ikiwemo maombi ya nyongeza ya fedha yaliyotokana na ucheleweshaji malipo kwa hati tatu za madai ulisababisha mkataba huo kuvunjwa mnamo mwezi Juni 2021 na kutokana na umuhimu wa mradi huo tarehe 13 /6/2022 wizara ilisaini mikataba miwili kwa ajili ya kukamilisha mradi huo ambapo chuo kiliendelea kutekeleza ujenzi wa makataba kwa kutumia Wakala wa Majengo Tanzania (TBA) akiwa mkandarasi mshauri.
Naibu Waziri wa Ardhi Nyumba na Maendeleo ya Makazi Mhe. Geophrey Pinda akisisitiza jambo kwa Kaimu Mkuu wa Chuo cha Ardhi Morogoro Juma Mkuki alipofanya ziara kwenye chuo hicho tarehe 15 Juni 2024 mkoani Tabora.
Naibu Waziri wa Ardhi Nyumba na Maendeleo ya Makazi Mhe. Geophrey Pinda akimsikiliza Meneja wa Wakala wa Majengo Tanzania (TBA) mkoa wa Tabora Mhandisi Ebenezer Ngure wakati wa ziara yake ya kukagua ujenzi wa mradi wa Maktaba ya Chuo cha Ardhi Tabora tarehe 15 Juni 2024 mkoani Tabora.
Naibu Waziri wa Ardhi Nyumba na Maendeleo ya Makazi Mhe. Geophrey Pinda akisalimiana na Kamishna wa Ardhi Msaidizi mkoa wa Tabora Huseni Sadick mara baada ya kuwasili Chuo cha Ardhi Tabora kwa ajili ya ziara ya kukagua maendeleo ya ujenzi wa Maktaba ya chuo pamoja na kuzungumza na watumishi tarehe 15 Juni 2024 mkoani Tabora. (PICHA ZOTE NA WIZARA YA ARDHI)