Naibu Waziri wa Nishati, Mhe. Judith Kapinga amesema Serikali kupitia Shirika la Umeme Tanzania(TANESCO) inatekeleza Mradi wa Njia ya Kusafirisha Umeme wa Msongo Mkubwa wa Kilovolti 400 wa Tanzania na Zambia (TAZA) kupitia Iringa ambao utasaidia kuboresha huduma ya upatikanaji wa umeme katika Mji wa Mafinga na maeneo jirani.
Mhe. Kapinga amesema hayo Tarehe 18 Juni 2024, Bungeni Jijini Dodoma wakati akijibu swali la Mbunge wa Mafinga, Mhe. Kosato Chumi aliyetaka kufahamu Mpango wa Serikali wa kukabiliana na tatizo la umeme mdogo (Low Voltage) katika Mji wa Mafinga.
Amesema kupitia mradi huo, vitajengwa Vituo vya Kupokea na Kupoza Umeme katika maeneo mbalimbali ikiwa ni pamoja na eneo la Kisada kwa ajili ya kusambaza umeme katika mji wa Mafinga na maeneo jirani.
Mradi huo pia utaondoa tatizo la kuzidiwa uwezo katika njia ya kusafirisha umeme yenye urefu wa Kilomita 90 kutoka kituo cha Mafinga hadi Mgololo.
Akizungumzia kuhusu Serikali kuigawa Wilaya ya Mufindi ili kuwa na Wilaya mbili za Kitanesco zitakazo hudumia Mufindi na Mafinga Mjini, Mhe. Kapinga amesema kuwa Wizara ya Nishati inalifanyia kazi suala hilo na kuona namna bora ya kuboresha huduma katika eneo husika.
Aidha, ameendelea kusema kuwa katika mwaka ujao wa fedha, Wizara imetenga bajeti ya kupeleka umeme katika Vitongoji 4,000 ikiwemo vya Mji wa Mafinga.
Katika hatua nyingine akijibu swali la Mbunge wa Busanda Mhe. Bryceson Maggesa Tumaini aliyetaka kufahamu hatua ambazo Serikali inachukua kuongeza kasi ya Wakandarasi kutekeleza miradi ya umeme Jimboni Busanda, Mhe. Kapinga amesema Serikali kupitia Wakala wa Nishati Vijijini (REA) inaendelea na Utekelezaji wa Mradi wa Usambazaji wa Umeme katika maeneo yaliyopembezoni mwa Miji( Per Urban) kupitia Mkandarasi ambaye ni Kampuni Tanzu ya TANESCO inayohusika na ukarabati wa miundombinu ya Usafishaji na Usambazaji wa Umeme(ETDCO) ambapo utekelezaji wake umefikia asilimia 47 na unaendelea vizuri.
Vilevile REA inatekeleza mradi wa kupeleka umeme kwa Wachimbaji wadogo (Small Scale Mining, Industrial and Agricultural Area) ambao ulianza kutekelezwa mwezi Aprili.
Amesisitiza kuwa mpango wa Serikali ni kuhakikisha Taasisi zote za Serikali na zisizo za Serikali zinapata umeme kadri ambavyo miradi ya kusambaza umeme Vijijini na Vitongojini inavyotekelezwa na tayari Serikali ina mpango wa kuongeza nguvu ya Umeme katika maeneo ya vijijini yanayopara Umeme Mdogo.