Waziri Mkuu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Kassim Majaliwa ameziagiza Wizara ya Madini na Wizara ya Nchi, Ofisi ya Rais, Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (TAMISEMI) kupitia Sheria Ndogo za Halmashauri ili kuondoa changamoto wanazokumbana nazo Wachimbaji Wadogo wa Madini.
Ametoa maagizo hayo leo Juni 27, 2024 wakati akifunga Wiki ya Madini kwa mwaka 2024 iliyokwenda sambamba na maonesho ya madini na vifaa vya uchimbaji, mkutano wa FEMATA na kongamano la wachimba Madini yaliyofanyika kuanzia tarehe 20 – 27 Juni, 2024, katika Viwanja vya Ukumbi wa Mikutano wa Jakaya Kikwete jijini Dodoma.
Waziri Mkuu Majaliwa amesisitiza, Wizara ya Madini na TAMISEMI kupitia sheria ndogo za Halmashauri zinazowaletea changamoto wachimbaji wa madini ili kufanya marekebisho yatakayowawezesha wachimbaji kuendelea kuchimba kwa amani na tija zaidi na hatimaye kuongeza mchango wao katika maendeleo ya Sekta ya Madini.
Aidha, amewataka wachimbaji wa madini kuzingatia Sheria, Kanuni, na taratibu za uchimbaji madini ili kulinda mazingira na kueleza kuwa, Serikali itaendelea kushirikiana na FEMATA ili kuendeleza na kukuza uchumi wa madini nchini.
Katika hatua nyingine, Mhe. Majaliwa ametoa wito kwa taasisi za elimu kufanya maboresho ya mitaala kuhusu sekta ya madini ili kuendana na mahitaji ya sasa kutokana na mabadiliko makubwa ya kiteknolojia sambamba na uhitaji wa madini muhimu duniani kote, jambo litakalosaidia katika kuhamisha nguvu kulekea kwenye soko la madini mkakati na nishati mbadala.
Pia, amewahimiza wachimbaji wa madini kuendelea kutumia Vision 2030: Madini ni Maisha na Utajiri, maono ambayo kupitia Taasisi ya Jiolojia na Utafiti wa Madini Tanzania (GST), Wizara imepanga kufanya utafiti wa kina (High-Resolution Airborne Geophysical Survey) wa miamba yote yenye madini iliyopo hapa nchini, ili kupata taarifa za uhakika za aina ya madini yaliyopo nchini.
Kwa upande wake, Waziri wa Madini Mhe. Anthony Mavunde amesema Wizara inaendelea kuchukua hatua mbalimbali ili kuongeza tija katika sekta ya madini ikiwa ni pamoja na kuwapa wachimbaji wadogo maeneo ya kuchimba na kuwapatia leseni ili wafanye uchimbaji bila usumbufu sambamba na kufuta leseni zote zisizofanyiwa kazi au kuendelezwa, na kuondoa maombi mengi ya leseni ili kutoa nafasi kwa watanzania kuchimba madini kwa tija.
Ameongeza kuwa, Wizara imeanzisha programu maalum ya Mining for a Brighter Tomorrow (MBT) kwa ajili ya kusaidia vijana na wanawake kwa kuwapatia maeneo ya kuchimba pamoja na vifaa ili waweze kujiajiri na kufanya kazi ya uchimbaji kwa ufanisi na tija zaidi.
Naye, Rais wa FEMATA, John Bina amesema kuwa kama Wachimbaji Wadogo, wamepanga baadhi ya mikakati ikiwemo kuwekeza katika la madini ya viwandani na madini mkakati na kwamba kwa muda mrefu wamewekeza katika kuchimba madini ya dhahabu na sasa wako tayari kuingia katika madini tofauti kutokana na kuongezeka kwa mahitaji ya madini hayo sambamba na upatikanaji wa soko la uhakika ulimwenguni kote.
Kwa upande wake, Mwenyekiti wa Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Nishati na Madini Mhe. David Mathayo ameilekeza Serikali kuhakikisha inafikisha huduma ya nishati ya umeme katika maeneo yote yenye shughuli za uchimbaji wa madini ili kupunguza gharama za uzalishaji.
Vilevile, ameiomba Serikali kuendelea kununua mitambo ya uchorongaji kwa ajili ya wachimbaji wadogo na kuhakikisha inayafikia maeneo yote kwa usawa.
Wiki ya Madini, Maonesho ya Madini na Vifaa vya Uchimbaji Madini yalikwenda sambamba na Kongamano la Wachimbaji na Mkutano wa Shirikisho la Vyama vya Wachimbaji Wadogo wa Madini Tanzania ( FEMATA ambako lilifunguliwa na Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt. Philip Mpango Juni 20, 2024.