Breaking

Thursday, 13 June 2024

MABORESHO MAKUBWA SEKTA YA UTALII HAYA HAPA



Na John Mapepele

Serikali imependekeza kufanya marekebisho makubwa kwenye Kanuni ya Ada na Tozo za Utalii ya mwaka 2015 ili kuleta mapinduzi makubwa kwenye sekta ya utalii.

Akisoma hotuba yake wakati akiwasilisha bungeni mapendekezo ya Serikali kuhusu makadirio ya mapato na matumizi kwa mwaka 2024/2025 , Waziri wa Fedha, Mhe. Dkt, Mwigulu Nchemba ameyataja marekebisho kuwa ni pamoja na; kutoza ada ya Leseni za Biashara za utalii kwa shilingi za Tanzania badala ya dola za Marekani.

Amesema mapendekezo haya yanakwenda sambamba na kuweka takwa la ada hizo kulipwa katika kipindi cha miezi 12 kuanzia siku ya malipo ya mwisho ya leseni ya biashara yalipofanyika.

Pia kupunguza ada ya leseni ya biashara ya utalii inayolipwa na Wakala wa wapandisha watalii mlimani kutoka dola za Marekani 2000 kwa mwaka hadi shilingi milioni 3 za Tanzania kwa mwaka.

Amefafanua kuwa lengo la hatua hizo ni kurahisisha mfumo wa ulipaji wa ada za utalii, kupunguza gharama za uendeshaji, kuvutia uwekezaji katika tasnia ya utalii na kuendana na matakwa ya kifungu cha 26 Cha Sheria ya Benki Kuu ya Tanzania kinachoelekeza malipo yanayofanywa nchini kutumia shilingi ya Tanzania.
Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia langolahabari@gmail.com au WhatsaApp: +255 621 896 990

Pages