Breaking

Sunday 23 June 2024

MABAHARIA DMI WAUNGANA NA MABAHARIA NCHINI KUFANYA USAFI BAGAMOYO

TIMU ya mabaharia kutoka Chuo Cha Bahari Dar es Salaam -DMI, Leo wameungana na mabaharia nchini kwa kufanya usafi katika baadhi ya fukwe zilizopo Bagamoyo katika Mkoa wa Pwani ikiwa ni mwendelezo wa kuadhimisha Siku ya Mabaharia Duniani.

Mabaharia hao wamekuwa mfano kwa wadau mbalimbali wa tasnia ya bahari kwa kufanya usafi katika fukwe za Kaole na Soko la Samaki zilizopo Bagamoyo sambamba na kukutana na wavuvi wadogo wadogo ili kuhamasisha umuhimu wa usafi katika fukwe za bahari, kuhakikisha wanakuwa na vifaa vya uokozi wakiwa baharini, kuwa na vifaa vya mawasiliano katika vyombo vyao pia wawe na mazoea ya kukagua vyombo vyao kwa ajili ya usalama majini.

Katika ziara hiyo iliyoratibiwa na Wizara ya Uchukuzi, ilihusisha Serikali katika eneo husika ambapo mabaharia hao waliweza kukutana na wananchi walioshiriki zoezi la usafi pamoja nao lakini pia walitoa elimu juu ya umuhimu wa kutunza mazingira hususan katika fukwe za bahari pamoja na usalama wawapo baharini.

Mabaharia wamezidi kusisitiza kutambua mchango wao duniani na kitaifa hususan katika nyanja za kibiashara, uchumi na jamii kwa ujumla kwa kuhakikisha jamii inakuwa na matumizi sahihi ya bahari katika mbio za kuufikia uchumi wa bluu.
Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia langolahabari@gmail.com au WhatsaApp: +255 621 896 990

Pages