Breaking

Saturday, 1 June 2024

KUTANA NA WISDOM A. MOLA MSOMI WA CHUO KIKUU ALIYEONA FURSA KATIKA SEKTA YA KILIMO.

(Kutoka kituo cha utafiti, TARI Ukiriguru- Mwanza)

Wisdom A. Mola msomi kutoka Chuo Kikuu cha Kilimo Sokoine (SUA) Morogoro, alimaliza shahada ya kwanza ya sayansi ya kilimo biashara mwaka 2013.

Baada ya kuhitimu shahada hiyo aliamua kujikita katika biashara ya mazao hususani kutengeneza mnyororo wa thamani kwa kuyaongezea thamani mazao yake.
Anasema alianza kuwa na ndoto za kuwa mfanyabiashara tangu akiwa anasoma chuo kikuu, na alianza kwa kufanya biashara ya boda boda iliyokuwa inamuingizia kipato kipindi akiwa anaendelea na masomo yake ya elimu ya juu.

Wakati anamaliza masomo yake ya elimu ya juu, Wisdom alianza kutafuta kazi za kuajiriwa na baada ya kukosa ajira alianza kuumiza kichwa ni namna gani anaweza kujikwamua kimaisha na ndipo wazo la kuanzisha kampuni ya kuchakata mazao ya kilimo likamjia.
Anasema, baada ya kupata wazo hilo aliwashirikisha vijana wenzake kutoka katika vyuo vingine ili kuona ni namna gani wanaweza kuunganisha mawazo yao na kuwa na wazo moja la uwekezaji.


Walianza kufanya tafiti ndogo kwenye baadhi ya mikoa na ndipo wazo la kwanza likawa uwekezeshaji wao waufanyie mkoani Geita katika Wilaya ya Bukombe na hapa ndipo ndoto yao ikaanza kutekelezwa ili kufikia malengo yao.“Wazo la kuanza biashara ya uchakataji wa mazao ya kilimo iliambatana na uanzishwaji wa kampuni ya BORA FOOD KILIMO BIASHARA ambayo ilianza mnamo April, 2014.


"Fursa ya kuanzisha uchakataji wa mazao ya kilimo ulitokana na kuona ni namna gani tunaweza kupunguza athari ya upotevu wa chakula, ambapo zaidi ya asilimia 70 ya mavuno kutoka shambani yanapotea wakati wa kuvuna na kuhifadhi. Kwa wakati huu kampuni ilianza uchakataji wa mazao ya kilimo yakiwemo mpunga, mahindi na baadaye karanga, muhogo na alizeti” anasema.


Wisdom anasema kuwa wakati wanaanza biashara hii hawakuwa na mtaji wa kutosha, walitegemea fedha kutoka kwa ndugu na marafiki wa karibu ili waweze kuendeleza na kufanikisha wazo la biashara ya uchakataji wa mazao ya kilimo.“Wakati tunaanza tulianza na mtaji wa Tsh. 8,000,000=, mwanzoni tulinunua mashine za kuchakata mpunga na mahindi zilizokuwa zinatumia nishati ya mafuta (dizeli), kwa wakati huo eneo la mradi lilikuwa halijafikiwa na umeme.


Kufikia mwaka 2018 serikali iliweka umeme katika eneo la Runzewe wilayani Bukombe na ndipo jukumu la kubadilisha mashine kutoka kutumia nishati ya mafuta na kuanza kutumia nishati ya umeme lilifanyika” .Baada ya mafanikio makubwa katika uchakataji wa mazao hususani mpunga na mahindi Wisdom A. Mola na wenzake katika kuhakikisha kuwa wanatengeneza wigo mkubwa katika sekta ya kilimo kupitia uchakataji wa mazao, kampuni ilianzisha uchakataji wa zao la muhogo.

Anasema katika kuliongezea thamani zao la muhogo, walipata fursa ya kuhudhuria mafunzo ya uzalishaji wa mbegu bora za muhogo kupitia kituo cha Utafiti wa Kilimo cha TARI Ukiriguru (Mwanza) kwa kushirikiana na shirika la MEDA na Taasisi ya Kimataifa ya Utafiti wa Kilimo Ukanda wa Kitropiki (IITA) lengo likiwa ni kuliongezea thamani zao hilo lililokuwa limesahaulika kipindi cha nyuma kutokana na wakulima wengi kukosa na kutotumia teknolojia mpya za mbegu bora zinazotoa mavuno mengi pia zenye uvumilivu dhidi ya magonjwa ya Batoto kali na Michirizi kahawia ikilinganishwa na mbegu za kienyeji.

Katika kuhakikisha mkulima analima kwa tija, walihakikisha mbegu bora za muhogo zikiwemo TARICASS1, TARICASS 2, TARICASS3, TARICASS4, TARICASS5, Kiroba, Mkuranga 1, Kizimbani na nyinginezo zinawafikia wakulima kwa muda mwafaka. Anaendelea kwa kusema kwa sasa kampuni imeamua kufanya kazi na wakulima wa zao la muhogo ili kuwasaidia kupata mikopo midogo yenye riba nafuu itakayowasaidia kufanya kilimo kwa tija kubwa na kuwahakikishia soko kwa kununua mihogo yao.

Kwa upande wa mafanikio ya kampuni ya “BORA FOOD KILIMO BIASHARA”, imepiga hatua kubwa sana kutoka kuwa tegemezi na sasa kampuni imeweza kujiendesha kwa asilimia 100. Kampuni ilianza shughuli zake ikiwa na mtaji wa shilingi milioni nane (Tsh. 8,000,000=) ambao umekuwa na kufikia thamani ya shilingi milioni mia tatu (Tsh. 300,000,000=) hii inatokana na kuaminiwa na taasisi za kifedha zinazowapatia mikopo yenye riba nafuu hususani mikopo kutoka ofisi ya Waziri mkuu kupitia Halmshauri ya Wilaya kwa ajili ya walemavu, wanawake na vijana.

“Napenda kuishukuru Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kupitia kwa Rais Dkt. Samia Suluhu Hassani kwa kutuwezesha vijana kujiajiri na kupata mikopo mbalimbali yenye unafuu ambayo inasaidia kujikwamua kimaisha na pia kutengeneza mazingira salama ya kufanyia biashara...Niwatie moyo vijana wenzangu kwamba tatizo la ajira ni kubwa lakini wakiamua kujiajiri wanaweza kufanya vizuri zaidi, kuwa na uthubutu na wasiogope. Jambo lingine ni kuwa na nidhamu katika kazi na kuwa na malengo endelevu yatakayo wawezesha kufanikisha kwenye kila hatua.” anasema Wisdom A. Mola ambaye ni Mkurugenzi mtendaji wa BORA FOOD KILIMO BIASHARA.
Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia langolahabari@gmail.com au WhatsaApp: +255 621 896 990

Pages