Naibu Waziri wa Nishati, Mhe. Judith Kapinga amesema changamoto ya umeme katika Mkoa wa Rukwa itamalizika baada ya Mkoa huo kuunganishwa katika Gridi ya Taifa kupitia Mradi wa njia ya kusafirisha Umeme wa Msongo wa Mkubwa wa Kilovolti 400 wa Tanzania - Zambia (TAZA).
Mhe. Kapinga amesema hayo leo Juni 26, 2024 Bungeni Jijini Dodoma alipokuwa akijibu swali la Mbunge wa Nkansi, Mhe. Aida Khenani aliyetaka kufahamu mpango wa Serikali wa kumaliza changamoto ya umeme Wilaya ya Nkansi.
Amesema kupitia mradi huo kitajengwa Kituo vya Kupokea na Kupoza umeme cha Nkansi ambacho kitasaidia kuboresha upatikanaji wa umeme katika Wilaya hiyo na maeneo jirani.
Kuhusu mabadiliko ya bei za umeme katika Mamlaka za Miji Midogo za Namanyere na Laela, amesema kuwa Serikali imefanya mapitio na imeshauri kuwa maeneo 1,500 yamekidhi kulipia kiasi cha shilingi 27,000 badala 320,000.
Vilevile Serikali inaendelea kufanya mapitio katika maeneo mengine ya Miji hiyo ili kujiridhisha kama yanakidhi vigezo husika na ili yaingizwe kwenye malipo ya shilingi 27,000/-.
Kuhusu utekelezaji wa mradi wa TAZA, amesema kuwa, Naibu Waziri Mkuu na Waziri wa Nishati, Mhe. Dkt. Doto Biteko alifanya ziara katika mradi huo na kwamba utekelezaji wake unaenda kwa kasi na Serikali inaendelea kumsimamia Mkandarasi anayetekeleza mradi huo ili ukamilike kwa wakati.
Amesisitiza kuwa adhma ya Serikali ni kuyafikishia umeme maeneo yote muhimu zikiwemo Taasisi zilizopo umbali usiozidi mita 500 kutoka ilipo miundombinu ya umeme na kuongeza kuwa maeneo ambao yapo mbali na miundombinu hiyo yatafikiwa kupitia miradi ya vitongoji.