Breaking

Tuesday, 18 June 2024

DKT. HASHIL - BRELA IMEDHAMIRIA KUDUMISHA UHUSIANO MZURI NA VYOMBO VYA HABARI

NA EMMANUEL MBATILO, MOROGORO

KATIBU Mkuu wa Wizara ya Viwanda na Biashara, Dkt. Hashil Abdalah amewapongeza Wakala wa Usajili za Biashara na Leseni (BRELA) kwa kuweza kuandaa mafunzo kwa waandishi wa habari za biashara kwani wamedhamiria kudumisha uhusiano na mawasiliano na vyombo vya habari.

Ametoa pongezi hizo leo Juni 18,2024 Mjini Morogoro wakati wa Mafunzo ya siku nne ya BRELA kwa Waandishi wa Habari wanaoripoti Mkoa wa Dar es Salaam, yanayoendelea mkoani Morogoro.

Amesema BRELA imeona umuhimu wa kukaa na waandishi hao ambao ni nanyi wadau muhimu katika kuelimisha na kuhabarisha umma kuhusu namna Serikali inavyohudumia wananchi wake kupitia sekta ya biashara huku akisisitiza kwa kuifahamu BRELA itarahisisha hata vyombo vya habari kutoa taarifa sahihi za Wakala huo.

"Naamini mafunzo haya yataleta tija kwenu kwa kujua kwa kina majukumu, mafanikio, changamoto na ufumbuzi katika utekelezaji wa majukumu ya taasisi katika utoaji wa huduma bora kwa umma kwa kuzingatia mabadiliko ya teknolojia,”amesema Dk.Abdallah.

Katibu Mkuu huyo amewaomba wanahabari kupitia kalamu zao na vipaza sauti wasaidie katika kuhakikisha taarifa za BRELA zinatiliwa mkazo ili kuwezesha umma wa Watanzania kwa ujumla kuhamasika katika kurasimisha biashara zao ukizingatia urasimishaji wa biashara hizo zinafanyika kwa njia ya mtandao.

“Zipo changamoto nyingi ambazo wananchi wanakabiliana nazo kwenye hatua ya kufikia urasimishaji wa biashara, natambua ukuaji wa teknolojia huweza kuwa kikwazo lakini hatuwezi kusimama wakati dunia inakimbia kutokana na mabadiliko na ukuaji wa teknolojia. Hivyo, changamoto kama hizi ninyi waandishi ndipo taaluma yenu inapohitajika katika kuwaelimisha, kuwaelekeza na kuwaongoza umma.”

Pamoja na hayo amesema mategemeo yake kupitia mafunzo haya waandishi wa habari wataacha kuandika habari kwa mfumo wa mazoea kwasababu watakuwa na taarifa za kina kuhusu BRELA lakini kwa kupitia mafunzo hayo itakuwa ni mwanzo wa kuwaweka karibu na taasisi pindi unapohitaji ufafanuzi wa kina.

“Niwaombe uandishi wenu uzingatie matumizi mazuri ya lugha, kwa kuwa kila mtu anafahamu kuwa lugha ni kitu chenye uhai na kinaweza kutumika kwenye ubunifu katika uandishi, mzingatie matumizi mazuri ya rasilimali zote za lugha. Lugha hutuwezesha kutoa maoni, maelekezo, habari na hisia na kama mtumiaji wa lugha tunatambua kuwa ikitumiwa ipasavyo huleta uhai katika taaluma ya mawasiliano.

“Hivyo niwaombe waandishi wa habari, kwa kuwa masuala mengi ya BRELA yamekaa kisheria, waandishi mtumie lugha laini kuwaeleza wananchi ili waweze kufahamu kwa kina. Kwa lugha zenu za kitaalamu za uandishi mtaweza kuvunja vunja lugha pasipo kupotosho umma na mkumbuke kuwa jamii inawategemea katika hili.”

Amesema wapo waandishi wa habari wanaweza kuwa na mitazamo tofauti kwa namna wanavyotafsiri sheria za utekelezaji wa majukumu ya BRELA na kusababisha muda mwingine kuandika kichwa cha habari kinachopiga kelele au kichwa cha habari kinachohukumu (judgemental headline) na kuleta taharuki kwa umma.

“Naamini kupitia mafunzo haya mtaelekezana kwa kina yale ambayo yamekuwa kigugumizi kwenu kufuatia tafsiri mbalimbali na kupata majibu ya kina. Hata hivyo mkumbuke ibara ya 18 ya Katiba ya Muungano ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania inaeleza kuwa Kila mtu - (a)…

“Ana uhuru wa kuwa na maoni na kujieleza maoni au mawazo yake; (b) ana haki ya kutafuta, kupokea na, au kusambaza taarifa bila ya kujali mipaka ya nchi; (c) ana uhuru wa kuwasiliana na haki ya kulindwa dhidi ya kuingiliwa kati kwa mawasiliano yake; na (d) ana haki ya kupata taarifa wakati wote kuhusu matukio mbalimbali muhimu yanayoendelea kuhusu maisha na shughuli za wananchi, na pia juu ya masuala muhimu kwa jamii.

“ Hivyo, mtambue kuwa ibara hii inawalinda waandishi hawa katika utekelezaji wa majukumu yao kwa kutoa habari muhimu na zenye maslahi kwa umma na umma pia una haki ya kupata taarifa.Kutokana na hilo mtakuwa na jukumu kutoa habari kwa haraka bila kusitasita na kuleta ukakasi wanapokuwa wanatekeleza majukumu yao,”amesema Dk.Abdallah.

Ameongeza kuwa waandishi waelewe kuwa misingi yao ya habari inaelekeza kuweka habari kwa usawa (balancing of stories na kusisitiza anaamini mafunzo hayo yatafungua milango ya kuwa na mafunzo kwa waandishi wa habari katika mikoa mingine kwani BRELA inafanya kazi nchi nzima na kila mikoa ina waandishi hasa redio za kijamii ambazo zinasikika hadi ngazi ya kata.
Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia langolahabari@gmail.com au WhatsaApp: +255 621 896 990

Pages