Wateja wa huduma za Maji katika kata za Mwananyamala na Makumbusho katika Wilaya ya Kinondoni Jijini Dar es Salaam wametakiwa kulipa bili zao kwa wakati ili kuiwezesha DAWASA kuboresha zaidi huduma na kuwafikia wananchi wengi zaidi waliopo ndani ya eneo la kihuduma la Mamlaka.
Akiongea wakati wa zoezi la kufuatilia wadai wa huduma za majisafi wenye madeni ya muda mrefu kupitia Dawati la huduma kwa wateja, Afisa huduma kwa wateja mkoa wa kihuduma DAWASA Kinondon Frank Sulley amesema kuwa Mamlaka imeamua kuwafuata mitaani na kuongea na wateja wenye malimbikizo ya madeni ya huduma za Maji katika kata za Mwananyamala na Makumbusho
"Tumeamua kufungua Dawati la huduma kwa wateja katika Ofisi za Watendaji wa Serikali za mtaa ambao ni viongozi wa Wananchi tunaowahudumia ili kuwafikia Wananchi wengi ambao sio tu wana madeni ya muda mrefu lakini pia wenye changamoto za kihuduma wanasikilizwa na kupatiwa ufumbuzi." alisema
Aliongeza kuwa, Mamlaka inaendelea kuwakumbusha wateja kuwa ni wajibu wa kila mteja anayetumia huduma ya maji kuhakikisha analipa bili yake kwa wakati ili kuepusha hatua nyingine zaidi za kisheria kuchukuliwa.
Ndugu Sulley amesema kuwa kwa wateja ambao wana malimbikizo ya madeni ya huduma kuwa wanakaribishwa katika Ofisi za DAWASA zilizo karibu nao ili wapate nafasi ya kuingia mkataba wa namna ya kulipa madeni yao kwa awamu.
Kwa upande wake Mwenyekiti wa Serikali ya mtaa wa Minazini, Ndugu Deogras Zunda ameishukuru DAWASA kwa elimu iliyotolewa kwani imesaidia kupata ufumbuzi wa changamoto mbalimbali za kihuduma hususani kwa wateja wenye madeni ya muda mrefu.
"Hii elimu nzuri kwa kuwa imetusaidia kujua namna bora ya kulipa na kufahamu kuwa mteja anaweza kuingia makubaliano na Mamlaka katika kupunguza deni lake la Maji. Wengi wa wateja wanaodaiwa huogopa kufika DAWASA wakijua watasitishiwa huduma." alisema Mwenyekiti Zunda.
Naye mkazi wa mtaa wa Minazini, Bi. Khadija Zuberi ameiomba DAWASA kushughulikia changamoto zao kwa haraka na hata wakiwapigia simu wafike kwa wakati kwasababu maji yanavyomwagika yanatia hasara Serikali.
Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia langolahabari@gmail.com au WhatsaApp: +255 621 896 990
Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia langolahabari@gmail.com au WhatsaApp: + 255 621 615 613 au +255 621 896 990