Breaking

Thursday 20 June 2024

BODI YA TANESCO YAFURAHISHWA NA MAENDELEO YA MRADI WA JNHPP

Na Charles Kombe, Rufiji

Bodi ya Wakurugenzi wa Shirika la Umeme Tanzania (TANESCO) imefurahishwa na kupongeza wasimamizi wa mradi juu ya hatua za ujenzi wa mradi wa kufua umeme wa bwawa la Julius Nyerere (JNHPP).

Hayo yamebainishwa na Makamu Mwenyekiti wa Bodi hiyo Zuhura Bundala walipokua kwenye ziara ya wajumbe wa bodi hiyo kutembelea mradi huo Juni 19 wakiambatana na kaimu Mkurugenzi wa Shirika upande wa uzalishaji Mha. Abubakar Issa.

"Niwaambie watanzania kujivunia Serikali yao inayopenda nchi na wananchi maana huu mradi ni mkubwa. Naipongeza TANESCO kwa kuendelea kusimamia ujenzi wa mradi huu" amesema Bi. Bundala

Ameongeza kuwa "taarifa tuliyopewa na wataalamu ni kuwa, mradi huu kiujumla wake umekamilika kwa asilimia 98.01".

Kwa upande wake Kaimu Mkurugenzi Mtendaji usambazaji Mha. Abubakar Issa amesema kwa sasa Tanzania hakuna kabisa mgao wa umeme kutokana na kuwa na ziada ya umeme.

"Mwisho wa mwezi huu tunatarajia kuingiza mashine namba saba ambayo itakwenda kuongeza megawati 235 na kupelekea kituo hichi kuwa na uwezo wa kuzalisha megawati 705" amesema Mha. Issa.

Hii ni ziara ya kwanza ya bodi katika mradi huu ambapo imejionea hatua kubwa ya maendeleo ya ujenzi iliyofikiwa katika mradi huu.






Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia langolahabari@gmail.com au WhatsaApp: +255 621 896 990

Pages