Breaking

Saturday, 22 June 2024

BILIONI 18 KUPELEKA HUDUMA YA MAJI KIBAMBA

Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania imetenga kiasi cha Shilingi bilioni 18 wa ajili ya kuimarisha upatikanaji wa majisafi kwenye katika kata ya Mbezi ambayo itaenda kuhudumia wakazi takribani 144,000

Huu ni mojawapo ya utekelezaji wa mkakati wa Serikali ya awamu ya Sita ya kuboresha upatikanaji wa huduma ya Majisafi kwa mijini kwa asilimia 95 ifikapo mwaka 2025 kama inavyoeleza katika ilani ya Chama Cha Mapinduzi.

Akizungumza wakati wa mkutano wa hadhara na Wananchi wa eneo la Mbezi Msumi wakati wa ziara yake Mkoani Dar es salaam, Naibu Waziri wa Maji, mhandisi Andrew Kundo amesema kuwa uwekezaji huu ni mojawapo ya mkakati wa Serikali wa kuhakikisha eneo lote la Kibamba linapata majisafi na kwa uhakika.

Ameongeza Mhe. Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan amedhamiria kuhakikisha anawatua ndoo kichwani Wananchi wa Jimbo la Kibamba ikiwemo eneo la Msumi kwa kutenga jumla ya Bilioni 18 ambazo zitatumika kuboresha huduma ya majisafi.

Mhandisi Kundo amesema kuwa kata ya Mbezi ni moja ya eneo korofi ambalo wananchi wamekuwa kwenye changamoto ya maji kwa muda mrefu, hivyo ni wakati sahihi kupata huduma bora na ya uhakika ambapo ameelekeza uchimbwaji wa visima katika eneo la Msumi kama mpango wa muda mfupi wakati utekelezaji wa mradi huo wa Bilioni 13 ukiwa unaendelea.

Kwa upande wake, Mbunge wa Kibamba, Mhe. Issa Mtemvu amesema uhitaji wa Wananchi wa Jimbo la Kibamba ni huduma ya Maji iliyo bora hivyo ni faraja kusikia mipango ya kuboresha upatikanaji wa majisafi katika eneo hilo.

"Tunakushukuru Naibu Waziri kwa kufika katika eneo la Msumi ambalo ni kati ya maeneo yanayopatikana katika Jimbo la uchaguzi wa Kibamba, Tunaamini ujio wenu unakwenda kutupa suluhisho la hutaki letu la muda mrefu."ameeleza

Nae Kaimu Afisa Mtendaji Mkuu wa DAWASA, Ndugu Kiula Kingu amesema kuwa DAWASA imepanga kutekeleza mradi huo utakaohusisha ujenzi wa tenki la Lita milioni 6 pamoja na kituo cha kusukuma maji eneo la Kibamba ambao pia utanufaisha eneo la Mbezi Msumi.

Ameongeza kuwa utekelezaji wa kazi hiyo utagharimu jumla ya Bilioni 13 huku pia kukiwa na fedha ya Tsh Bilioni 5 iliyotolewa na Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kwa ajili ya kuboresha huduma ya Maji katika mkoa wa Dar es Salaaam.

"Tunatambua changamoto iliyopo katika eneo hili, kama Mamlaka tayari tumeshafanya usanifu wa mradi ambao tunaamini unakwenda kutatua changamoto ya eneo hili"ameeleza.










Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia langolahabari@gmail.com au WhatsaApp: +255 621 896 990

Pages