Breaking

Friday, 14 June 2024

BASHUNGWA CUP 2024 KUANZA KURINDIMA MWEZI JULAI

Na Mathias Canal, Karagwe-Kagera

Mashindano ya mpira wa miguu yaliyopewa jina la "BASHUNGWA CUP 2024" yataanza kurindima mwanzoni mwa mwezi Julai 2024 katika Wilaya ya Karagwe mkoani Kagera.

Mashindano hayo yanayotarajiwa kufanyika kwa miezi miwili yatazinduliwa kata ya Iguruwa yakihusisha timu 77 kutoka vijiji 77 vya Halmashauri hiyo ambavyo vitaunda timu 23 kutoka kata 23 za jimbo hilo.

Akitoa maelezo ya awali wakati akikabidhi mipira 77 kwa kamati ya maandalizi ya mashindano hayo kwa niaba ya mbunge wa Jimbo la Karagwe, katibu wa Mbunge wa Jimbo la Karagwe Ndg Ivo Ndisanye amesema kuwa mashindano hayo yatakuwa na lengo mahususi ambalo ni kutekeleza kwa vitendo ilani ya uchaguzi ya CCM ya mwaka 2020-2025 inayobainisha umuhimu wa michezo.

Ameyataja malengo mengine katika mashindano hayo kuwa ni kuimarisha afya kwa vijana, Kusaka vipaji na kuviendeleza kwa kuunda timu ya Halmashauri itakayoshiriki katika ligi mbalimbali ndani na nje ya wilaya ya Karagwe.

Kwa upande wake Mwenyekiti wa mashindano hayo Anastazia Amani ambaye pia ni Katibu wa Wazazi Wilaya ya Karagwe, amesema kuwa jambo hilo ni utekelezaji wa ilani ya CCM kwa vitendo kwani mashindano hayo yatatoa fursa ya serikali kueleza mafanikio ya awamu ya sita inayoongozwa na Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe Samia Suluhu Hassan.

Amesema kuwa serikali inafanya kazi kubwa ikiwemo uimarishaji wa miradi ya maji, miundombinu, elimu, afya na uwekezaji hivyo michezo ni sehemu ya fursa muhimu kuwakutanisha pamoja wananchi na kueleza utekelezaji wa ilani ya CCM.
Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia langolahabari@gmail.com au WhatsaApp: +255 621 896 990

Pages