Breaking

Friday, 28 June 2024

AMERICARES YATOA MATIBABU BILA MALIPO KWA WAGONJWA WA FISTULA MKOANI SHINYANGA

 


Na Mwandishi wetu - Malunde 1 blog

Shirika la Americares limeendesha zoezi la utoaji wa huduma ya matibabu ya bila malipo na kufanya operesheni ya ugonjwa wa fistula kwa kina mama waliobainika kuwa na ugonjwa huo ndani ya mkoa wa Shinyanga.

Zoezi hilo la matibabu limefanyika kwa muda wa siku tatu katika hospitali ya Rufaa ya Mkoa wa Shinyanga iliyopo kata ya Mwawaza manispaa ya Shinyanga.

Mratibu wa zoezi hilo la matibabu bi. Halima Khamis ambaye pia ni Mratibu wa Afya ya Uzazi ya Mama na Mtoto Mkoa wa Shinyanga amesema kufuatia uwepo wa malalamiko na changamoto ya ugonjwa wa fistula kwa baadhi ya akina mama mkoani humo ndipo walichukuwa hatua na kuamua kusogeza huduma hiyo.

“Kutokana na uwepo wa malalamiko na changamoto ndipo tukachukua hatua kama Wizara ya Afya pamoja na ofisi ya mkuu wa mkoa kwa kushirikiana na wadau wetu Americares na hospitali ya kanda Bugando tukaona tuweke kambi hii ili kuwafikia Akina mama wenye ugonjwa wa fistula ambapo mpaka sasa tumefanikiwa kupata akina mama 24 waliojitokeza kwa ajili ya kupatiwa matibabu ya upasuaji wa ugonjwa huu.

“Pamoja na kutoa elimu ya afya tuliweza kutoa matangazo kupitia vyombo vya habari ambapo mpaka sasa tumepata Akina mama 24 waliojitokeza kwa ajili ya kupatiwa matibabu ya upasuaji wa ugonjwa wa fistula”, ameongeza Halima Khamis.

Mwakilishi kutoka Shirika hilo la Americares Dkt. Jonas Kagwisage, amesema wana miaka 13 sasa wamekuwa wakitoa huduma hiyo ya Matibabu bure ya Fistula kwa wanawake kwa kushirikiana na Madaktari Bingwa wa wanawake kutoka Hospitali ya Rufaa ya Bugando, na sasa wamefanya kambi mkoani Shinyanga kutoa huduma hiyo.

Amesema katika Mkoa wa Shinyanga wameanza Kambi hiyo tangu Juni 23 na itahitimishwa kesho Juni 29,2024 na kwamba hadi sasa wameshawafanyia Upasuaji wa Ugonjwa huo wa Fistula wanawake 16 na leo watawafanyia wengine nane na kufikisha idadi ya wanawake 24.


Daktari Bingwa wa Magonjwa ya Wanawake kutoka Hospitali ya Rufaa Bugando Jijini Mwanza Dk. Elieza Chibwe, amesema tatizo la Ugonjwa wa Fistula bado ni kubwa sana kwa wanawake na husabishwa na uchungu pingamizi kwa mwanamke anapokuwa mjamzito, na hutokea Tundu ambalo linaunganisha njia ya uzazi na sehemu ya haja kubwa na ndogo na Mwanamke hutokwa na haja kubwa na ndogo muda wote.


“Ugonjwa huu husababishwa na uzazi pingamizi wakati wa kujifungua au kutopata huduma kutoka kwa mtaalam wakati wa kujifungua kwa maana ya kujifungulia nyumbani au kujifungua bila msaada wa mtaalam na kupelekea kupasuka kwa njia ya uzazi na kusababisha kutoka haja ndogo mfululizo, ugonjwa wa Fistula ni ugonjwa wa Aibu na Matibabu ya Fistula ni Upasuaji tu, na tunataka hadi kufikia 2030 tatizo la Fistula liwelimekwisha kabisa,”amesema Dkt. Chibwe.

Naibu Meya wa Manispaa ya Shinyanga Zamda Shabani, amelishukuru Shirika la Americares kwa kufadhili wa Tiba hiyo, pamoja na Madaktari kutoka Bugando na kutoa wito kwa wanawake wajitokeze kwa wingi kupata huduma hiyo,ili waondokane na tatizo hilo na kufanya shughuli zao kwa uhuru huku Diwani wa Mwawaza Juma Nkwabi, ameiomba Serikali ipeleke pia Madaktari Bingwa wa kutoa huduma ya Fistula katika Hospitali hiyo ya Rufaa ya Mkoa wa Shinyanga, na kutotegemea Madaktari wa Bugando.

Naye Mmoja wa wanawake ambaye amefanyiwa upasuaji Terezia Mayunga kutoka wilayani Kahama, amesema ameishi na tatizo la Fistula kwa miaka 38, lakini sasa amepatiwa Tiba na hali yake ni nzuri, huku mwingine akibainisha kwamba baada ya kupatwa na tatizo hilo mumewake alimkimbia na sasa amepona na kushukuru Shirika la Americares na Madaktari kwa kumpatia tiba bure.

Daktari Bingwa wa Magonjwa ya Wanawake kutoka Hospitali ya Rufaa Bugando Jijini Mwanza Dk. Elieza Chibwe akizungumza.

Mwakilishi kutoka Shirika hilo la Americares Dk. Jonas Kagwisage akizungumza.

Mganga mfawidhi hospitali ya Rufaa mkoa wa Shinyanga Dkt. Luzila John akizungumza hospitalini hapo.



Kaimu Mganga Mkuu wa Mkoa wa Shinyanga Dkt. Faustine Mlyutu akizungumza wakati wa zoaezi hilo.

Kaimu Mganga Mkuu wa Mkoa wa Shinyanga Dkt. Faustine Mlyutu akizungumza wakati wa zoaezi hilo.

Naibu Mstahiki Meya Manispaa ya Shinyanga Zamda Shabani akizungumza wakati wa zoezi hilo.

Diwani kata ya Mwawaza Juma Nkwabi akizungumza wakati wa zoezi hilo.



Baadhi ya waliopatiwa matibabu








Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia langolahabari@gmail.com au WhatsaApp: +255 621 896 990

Pages