Breaking

Tuesday, 28 May 2024

WAZIRI SILAA AFUNGA OFISI YA MASIJALA YA ARDHI JIJI LA DODOMA

Na Munir Shemweta na Eleuteri Mangi

Waziri wa Ardhi Nyumba na Maendeleo ya Makazi Mhe. Jerry Silaa amefunga Masijala ya Ardhi ya Jiji la Dodoma ikiwa ni hatua ya wizara yake kuondoa changamoto za sekta ya ardhi katika jiji la Dodoma.

‘’Tumeamua kufunga masijala hii ya jiji, nimetoka kuweka makufuli tumeifunga. Tunahamisha shughuli hizi za ardhi kutoka hapa kuja ofisini kwangu kwa Waziri wa Ardhi. Na shughuli hizi tumezitoa hapa kwa sababu huyu aliyenyoosha mkono wa mwaka 2017 nikimpa nafasi aelezee mimi nakosa majibu kama waziri mwenye dhamana ya ardhi’’ Amesema Mhe. Jerry Silaa.

Akizungumza na wananchi baada ya kufunga makufuli kwenye masijala ya ofisi ya ardhi jiji la Dodoma tarehe 28 Mei 2024 Mhe. Silaa amemuelekeza katibu Mkuu wa wizara hiyo kusimamia shughuli hiyo ili kuhakikisha watu wanapata haki zao.

‘’Dkt. Samia ametuelekeza tusimamie haki za watu wake, na kazi hiyo tutaifanya kwa uadilifu mkubwa na ukisoma vitabu vyote vya vinaelezea kazi ya haki ni kazi ya kimungu’’ amesema Mhe. Silaa.

Amewaambia wananchi waliokwenda kupata huduma wakati wa kufunga ofisi hizo za masijala ya ardhi ya jiji la Dodoma kuwa, ofisi za ardhi sasa zitafunguliwa rasmi siku ya jumatatu tarehe 3 Juni 2024 kweye ofisi za ardhi iliopokuwa ofisi za halmashauri ya jiji la Dodoma zamani.

Aidha, amesema, wizara yake itajenga ofisi ya kisasa yenye Kamera zenye uwezo wa kuchukua sauti itakayosimamiwa moja kwa moja na ofisi ya waziri pamoja na Katibu Mkuu sambamba na kuweka maafisa waadilifu.

‘’Naenda kujenga ofisi ya kisasa itakuwa na jicho langu mimi moja kwa moja tutaweka maadfisa waadilifu binadamu wa siku hizi siyo binadamu wa zamani tutaweka kamera zitachukua picha na sauti na wakati nikiwa Dar es Salaam na jimboni katika ziara nina uwezo wa kuingia kwenye simu yangu kuangalia ofisi za ardhi dodoma wanafanya nini’’ amesema Mhe. Silaa.

Kwa mujibu wa Waziri Silaa, muelekeo wa Wizara ya Ardhi ni kujenga ofisi za kisasa ambazo wananchi watakuwa wakipata huduma kwa wakati mmoja usiokuwa na vyumba vya kujifungia.

Awali akiongea na watumishi wa ardhi ofisi ya jiji la Dodoma katika ofisi ya kamishna wa Ardhi Msaidizi mkoa wa Dodoma Mhe. Silaa amewataka watumishi hao kuwajibika wakati wa kutekeleza majukumu yao ya msingi ya kila siku ya kuwahudumia wananchi kwenye sekta ya ardhi.

Kwa upande wake Naibu Waziri wa Ardhi Nyumba na Maendeleo ya Makazi Mhe. Geophrey Pinda amewataka watumishi hao wa sekta ya ardhi kuwa tayari na kupokea mabadiliko yenye utendaji kazi wenye tija yatakayoleta uhai katika maisha ya watu.

‘’Daima lazima akili yako ihisi kwamba badiliko lolote kwako ni darasa’’ amesema Mhe. Pinda
Waziri wa Ardhi Nyumba na Maendeleo ya Makazi Mhe. Jerry Silaa (Kulia) akifunga kufuli kwenye ofisi ya Masijala ya Ardhi ya jiji la Dodoma alipokwenda kuzifunga rasmi ofisi hizo tarehe 28 Mei 2024.
Waziri wa Ardhi Nyumba na Maendeleo ya Makazi Mhe. Jerry Silaa (Kulia) akimkabidhi fungua Katibu Mkuu Mhandisi Anthony Sanga mara baada ya kuzifunga ofisi ya Masijala ya Ardhi ya jiji la Dodoma tarehe 28 Mei 2024.
Waziri wa Ardhi Nyumba na Maendeleo ya Makazi Mhe. Jerry Silaa (Katikati) akizungumza na wananchi mara baada kufunga ofisi ya Masijala ya Ardhi ya jiji la Dodoma tarehe 28 Mei 2024. Kushoto ni Katibu Mkuu Mhandisi Anthony Sanga na kulia ni Naibu Katibu Mkuu Lucy Kabyemera.
Waziri wa Ardhi Nyumba na Maendeleo ya Makazi Mhe. Jerry Silaa akizungumza na wananchi baada kufunga ofisi ya Masijala ya Ardhi ya jiji la Dodoma tarehe 28 Mei 2024. 

(PICHA ZOTE NA WIZARA YA ARDHI)
Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia langolahabari@gmail.com au WhatsaApp: +255 621 896 990

Pages