Breaking

Friday, 24 May 2024

WAZIRI KAIRUKI AMPONGEZA RAIS SAMIA KUTOA MAGARI KWA KANDA ZOTE ZA TFS NCHINI, KUWA KINARA WA NISHATI SAFI AFRIKA


Na John Mapepele

Waziri wa Maliasili na Utalii, Mhe Angellah Kairuki amempongeza Rais wa Jamhuri wa Muungano wa Tanzania, Mhe.Dkt. Samia Suluhu Hassan kwa kutoa magari 22 kwa Wakala wa Huduma za Misitu Tanzania (TFS) yatumike kwenye usimamizi wa rasilimali za misitu na nyuki nchini ili kuwakomboa wanawake waachane na nishati chafu za kuni na mkaa ambazo zimekuwa zikiwaletea changamoto nyingi na kinara wa matumizi ya nishati safi Afrika.

Mhe. Kairuki ametoa kauli hiyo leo Mei 2024 wakati alipokuwa akikabidhi kwa menejimenti ya TFS magari 22 yaliyonunuliwa na Serikali yatakayotumika katika usimamizi wa misitu katika kanda zote saba hapa nchini yenye thamani ya shilingi bilioni 4.3 ikiwa ni Toyota Prado VXL, 7 zilizogharimu shilingi bilioni 2.2 kwa ajili ya Wakuu wa Kanda hizo na Toyota LandCruiser Hardtop, 12 zilizogharimu shilingi bilioni 2.1 zitakazotumika na Maafisa kwenye maeneo yote ya kanda. Hiyo ikiwa ni awamu ya kwanza ambapo awamu ya pili serikali itatoa magari tisa aina ya Toyota LandCruiser Hardtop.

Amefafanua kuwa ukiachana na uharibifu wa mazingira unaotokana na matumizi ya nishati chafu ya kupikia kama kuni na mkaa tumeendelea kushuhudia majanga mengi yakitokea katika mazingira na afya ya binadamu ambapo mwanamke amekuwa mhanga mkubwa wa masuala haya kwa sababu kwa kiasi kikubwa ndiyo watafutaji na watumiaji wa nishati chafu za mkaa na kuni zinazotokana na ukataji wa misitu hivyo magari hayo yatasaidia kwenye doria na usimamizi wa rasilimali za misitu na nyuki.

Ameongeza kuwa kutokana na umuhimu huo, Mei nane mwaka huu, Mhe. Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan alizindua rasmi mkakati wa miaka 10 wa Taifa wa Matumizi ya Nishati Safi ya kupikia kutoka mwaka 2024 hadi 2034 unaohusisha pia masuala mbalimbali ikiwemo kuongeza uelewa wa wananchi kutumia Nishati Safi ambao umelenga kuhakikisha ifikapo mwaka 2030 zaidi ya asilimia 80 ya wanawake wote nchini waweze kutumia nishati safi.
Ametaka magari hayo yawe chachu ya kuwaongezea ari ya kufanya kazi kwa ubunifu, bidii na maarifa na kufika maeneo ya mbali zaidi huku wakiyatumia kwa uangalifu ili kuleta tija iliyokusudiwa ya kutoa elimu ya uhifadhi wa misitu, kufanya doria za kimkakati na kufanya usimamizi wa rasilimali za misitu kwa ujumla.

Aidha, ameitaka TFS kufikiria kuanzisha mazao mapya ya utalii wa ikolojia, miundombinu ya malazi kwa wageni na kuchangamkia biashara ya Cabon huku wakiendelea kuandika maandiko ya miradi ili kuliingizia fedha taifa.
Amesema ni muhimu kuthamini na kutekeleza kwa vitendo maono ya Mhe. Rais ya kutangaza Tanzania kama alivyofanya kwenye Filamu ya The Royal Tour na hivi Karibuni Filamu ya Amazing Tanzania iliyozinduliwa Beijing China Mei 15 mwaka huu.

Awali, akimkaribisha Mhe.Waziri Naibu Katibu Mkuu wa Wizara ya Maliasili na Utalii, CP Benedict Wakulyamba ambaye ndiye Msimamizi Mkuu wa Jeshi la Uhifadhi amemshukuru Mhe. Rais kwa kuendelea kuijengea uwezo TFS kwa kutoa fedha nyingi kununua vitendea kazi vya kisasa vya kufanyia kazi ya uhifadhi.

“Naomba niwe muwazi, katika kipindi chote cha utumishi wangu, katika kipindi hiki kifupi cha Mhe. Rais Samia amefanya maboresho ya kisasa kwa kusaidia kuleta vifaa vya kidigitali na magari, ninamshukuru na kumpongeza sana Mhe. Rais”. Ameongeza CP Wakulyamba

Kwa upande wake, Kamishna wa Uhifadhi wa TFS, Prof. Dos Santos Silayo amemhakikishia Waziri Kairuki kuwa Menejimenti yake imejipanga vizuri ili kuhakikisha kuwa magari hayo yatakwenda kuongeza ufanisi mkubwa na kuliingizia taifa mapato zaidi.

Amesisitiza kuwa kwa sasa TFS inatumia teknolojia ya kisasa ambayo itasaidia kuboresha usimamizi wa maeneo makubwa ya misitu na nyuki hapa nchini.

Hafla hiyo pia ilihudhuriwa na Mwakilishi wa Mwenyekiti wa Bodi ya TFS, Dkt. Siima Bakengesa, Mkurugenzi wa Idara ya Misitu na Nyuki wa Wizara ya Maliasili Deusdedith Bwoyo, Wasimamizi wa kanda zote saba za TFS na maafisa mbalimbali wa Wizara



Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia langolahabari@gmail.com au WhatsaApp: +255 621 896 990

Pages