Mamlaka ya Majisafi na Usafi wa Mazingira Dar es salaam (DAWASA) mkoa wa kihuduma Mkuranga, imepongezwa kwa kuimarisha huduma ya maji kwa wananchi katika kitongoji cha Kiloweko, kata ya Mipeko katika Wilaya ya Mkuranga.
Kuimarika kwa huduma ya maji kumetokana na kukamilika kwa ufungaji wa Transfoma mpya katika chanzo cha maji Mwanambaya ambayo imesaidia kutatua changamoto ya uwepo wa umeme mdogo (low voltage) na hivyo kupelekea kiwango cha kusukuma maji kwa wananchi kuwa hafifu.
Mwenyekiti wa Kitongoji cha Kiloweko , ndugu Zaharani Ridhiwani ameishukuru Serikali kupitia DAWASA kwa kutatua changamoto zinazohusu maji kwa wakati pale zinapojitokeza katika eneo lake.
"Tunashukuru Serikali na DAWASA kwa usikivu na uharaka wa kuendelea kuwajali wananchi, kipindi cha nyuma wananchi walikuwa wanapata shida ya maji kutokakana na changamoto ya umeme mdogo. Lakini DAWASA walipokea malalamiko hayo na kuyafanyia kazi na kwa sasa wananchi wanapata huduma ya maji kwa uhakika," aliongezea Ndugu Zaharani.
Naye Idd Madenge, mkazi wa Mwanambaya katika Kitongoji cha Kiloweko ameishukuru DAWASA-Mkuranga kwa kusikiliza kilio chao cha muda mrefu.
"Kukosekana kwa huduma ya maji ya uhakika katika makazi yetu ilikuwa ni changamoto ya muda mrefu, lakini kwa sasa tunaishuru serikali kwa kupitia DAWASA imetatua kilio chetu cha muda mrefu, ni jukumu letu wananchi kutunza miundombinu na vyanzo vya maji, pia naiomba DAWASA iendelee kuongeza huduma ya maji kwa maeneo ambayo bado ili wananchi waendelee kupata huduma ya maji bora na salama," amefafanua.
Kwa upande wake msimamizi wa mradi , Mhandisi Richard Katwiga amesema kufungwa kwa transfoma kumekuwa mkombozi kwa wananchi wa Mipeko na hivyo kuwasisitiza wananchi wanaohudumiwa na chanzo hicho kiendela kulinda miundombinu ya maji na kulipa ankara zao kwa wakati ili kusaidia upatikanaji wa huduma bora na endelevu.
L
"Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania inafanya jitihada nyingi katika kusogeza huduma kwa Wananchi ikiwemo huduma ya maji, hivyo kila mmoja ana wajibu wa kutambua jitihada hizi kwa kulinda miundombinu ya maji na kulipa ankara za maji wakati,” amesema.