Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Samia Suluhu Hassan anatarajiwa kufanya ziara katika Jamhuri ya Korea kuanzia tarehe 30 Mei 2024 hadi 6 Juni 2024 kwa mwaliko wa Rais wa Jamhuri ya Korea Mhe. Yoon Suk Yeol.
Akizungumza na Waandishi wa Habari Jijini Dar es Salaam leo tarehe 29 Mei 2024, Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Mhe. January Makamba (Mb.) amesema Mhe. Rais Samia ataanza ziara rasmi ya uwili nchini humo itakayofanyika tarehe 1 na 2 Juni 2024.
Ziara hiyo itafuatiwa na ziara ya kikazi itakayomuwezesha kushiriki Mkutano wa Wakuu wa Nchi na Serikali Kati ya Afrika na Korea utakaofanyika tarehe 3 na 4 Juni 2024.
Mhe. Makamba amesema, ziara rasmi ya Mhe. Rais Samia nchini humo, inalenga pamoja na mambo mengine kukuza na kuimarisha ushirikiano na uhusiano wa kisiasa na kidiplomasia katı ya nchi hizi mbili ambao umedumu wa miaka 32 sasa tangu ulipoanzishwa mwaka 1992.
Mhe. Makamba ameongeza kuwa, akiwa nchini humo, Mhe. Rais Samia atakutana kwa mazungumzo rasmi na mwenyeji wake Mhe. Rais Yoon Suk Yeol yatakayofanyika tarehe 2 Juni 2024..
Amesema mazungumzo hayo yatajikita kujadili namna ya kuimarisha ushirikiano kati ya Tanzania na Jamhuri ya Korea katika maeneo mbalimbali ikiwemo Afya, Elimu na Miundombinu.
Mhe. Makamba amesema wakati wa ziara hiyo, mikataba saba (7) ya kuimarisha ushirikiano katika sekta mbalimbali kati ya nchi hizi mbili itasainiwa. Ametaja Mkataba moja wapo unahusu msaada wa fedha kati ya Benki ya Exim ya Korea na Tanzania ambao utaiwezesha Tanzania kupata msaada na mkopo wa masharti nafuu wa Dola za Marekani Bilioni 2.5 ambao ni kwa ajili ya kugharamia miradi ya maendeleo kwa kipindi cha miaka mitano ijayo yaani mwaka 2024/2028.
Pia amesema Hati ya Makubaliano kati ya Taasisi ya Utafiti wa Madini Tanzania (GST) na Taasisi ya Sayansi ya Miamba na Madini ya Korea ambayo itahusu ushirikiano katika masuala ya utafiti, uchoraji ramani na shughili za maabara itasainiwa.
Hati ya Makubaliano nyingine itakayosainiwa itahusu ushirikiano kati Tanzania na Jamhuri ya Korea katika Maendeleo ya Uchumi wa Buluu huku Hati nyingine itakayosainiwa itahusu Utambuzi wa Vyeti vya Mabaharia.
Kadhalika amesema, Tamko la pamoja la kisiasa la uanzishaji wa majadiliano kuhusu Mkataba wa Ushirikiano katika masuala ya Uchumi litasainiwa pamoja na kusainiwa kwa Hati ya Makubaliano kati ya Wizara ya Madini ya Tanzania na Wizara ya Biashara, Viwanda na Nishati ya Jamhuri ya Korea kuhusu ushirikiano katika sekta ya madini kimkakati.
Pia ameongeza kuwa, Hati nyingine itakayosainiwa ni ile kati ya Shirika la Madini STAMICO na Shirika la Ukarabati wa Migodi na Rasilimali za Madini la Korea.
Pia amesema wakati wa ziara hiyo, Tanzania na Korea zitakubaliana kuanzisha ushirikiano na Chuo Kikuu cha Korea cha Aerospace kinachojishughulisha na masuala ya usafiri wa anga ikiwa na lengo la kuboresha soko la usafiri wa anga nchini na uendeshwaji na uratibu wa viwanja vya ndege, utaalam, utafiti na huduma ambapo Korea wanafanya vizuri katika eneo hilo.
Pia Mhe. Makamba amesema wakati wa ziara hiyo, Chuo Kikuu cha Korea cha Aerospace kitamtunukia Shahada ya Heshima ya Udaktari kwa kutambua mchango wake katika Menejimenti ya Usafiri wa Anga nchini.
Akizungumzia sehemeu ya pili ya ziara hiyo, Mhe. Makamba amesema itahusu ushiriki wa Mhe. Rais Samia kwenye Mkutano wa Wakuu wa Nchi wa Afrika na Korea utakaofanyika tarehe 3 na 4 Juni 2024.
Mhe. Makamba amesema wakati wa Mkutano huo, Mhe. Rais Samia atahutubia pamoja na kuzungumza katika moja ya majopo manne yatakayokuwepo ambayo yatahusu Ajira, Elimu, Mazingira na Mabadiliko ya Tabianchi na Miundombinu.
Mhe. Rais Samia pia atashiriki Mkutano utakaowahusisha Wakuu wa nchi wa Afrika na Wamiliki wa Kampuni kubwa za Korea ikiwemo Samsung, Hyundai ili kujadili fursa za kuwekeza barani Afrika ambapo pia Mhe. Rais Samia atakuwa na mazungumzo mahsusi na Kampuni kubwa za Korea kuhusu fursa za uwekezaji zilizopo hapa nchini.
Aidha, Mhe. Makamba ameongeza kuwa, katika kutambua maendeleo ya soko la filamu la Jamhuri ya Korea, Mhe. Rais Samia atazungumza na viongozi wa nchi hiyo wanaoshughulikia masuala ya sanaa, muziki na filamu ili kushirikiana nao katika kutangaza utamaduni wa Tanzania na kukuza sekta ya utalii na kuona namna ya kuanzisha Studio ya Filamu na Chuo cha Taifa cha Filamu hapa nchini.