Breaking

Tuesday, 7 May 2024

NYONGEZA YA SIKU ZA LIKIZO YA UZAZI WANAOJIFUNGUA WATOTO NJITI ITALETA TIJA SEHEMU ZA KAZI

07 Mei 2024, Dar es Salaam

Chama cha Wafanyakazi wa Serikali na Afya Tanzania (TUGHE) kimesema kuwa kimefurahishwa na Uamuzi wa Serikali wa kukubali ombi lililokuwa likiwasilishwa na Chama hicho la kuongeza Siku ya Likizo ya uzazi kwa Wafanyakazi Wanawake wanaojifungua watoto njiti kama ilivyotangazwa na Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Dkt. Philip Isdor Mpango alipokuwa Mgeni Rasmi wakati wa Kilele cha Maadhimisho ya Siku ya Wafanyakazi Duniani-Mei Mosi Kitaifa jijini Arusha.

Akizungumza na Waandishi wa Habari leo katika Tawi la TUGHE Hospitali ya Rufaa ya Temeke Jijini Dar es Salaam, Makamu Mwenyekiti wa TUGHE Taifa, Dkt. Jane Madete amesema kuwa Wafanyakazi wanawake wanaojifungua watoto njiti wanapitia changamoto mbalimbali ikiwemo za kiafya, hivyo wanahitaji kupata muda mwingi wa kupumzika na pia kumuhudumia mtoto toka katika kipindi cha uangalizi hadi wanaporuhusiwa kutoka hospitalini ndiyo maana Chama cha TUGHE kwa kutambua hilo kiliamua kubeba ajenda hiyo na kuiomba Serikali iweze kuongeza siku za likizo ya uzazi ili kuleta tija sehemu za kazi.

“Kufuatia uamuzi huu tunaiomba serikali sasa ianze mchakato wa kufanya marekebisho katika Sheria ya Ajira na Mahusiano kazini ambayo kwa sasa imekuwa ikitoa siku 84 kwa wanawake wanaojifungua mtoto mmoja na pia siku 100 kwa wanaojifungua zaidi ya mtoto mmoja. TUGHE tupo tayari kushiriki kikamilifu katika hatua zote za kuhakikisha uamuzi huu unaingia katika sheria hii” Alieleza Dkt. Madete

Kwa upande wa Sekta Binafsi, TUGHE imewaomba Waajiri nchini katika mikataba yao ya hali bora kuweka kipingele cha kuongeza muda kwa siku za likizo ya uzazi kwa wanaojifungua watoto njiti kama ambavyo mwishoni mwa mwaka jana 2023 Chama cha TUGHE waliweka kipengele hicho katika Mkataba wake wa Hali Bora na kuwa Chama cha kwanza cha Wafanyakazi Nchini kufanya hivyo katika Mkataba wake wa hali bora.

IMETOLEWA NA

IDARA YA HABARI NA UHUSIANO KWA UMMA

TUGHE MAKAO MAKUU
Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia langolahabari@gmail.com au WhatsaApp: +255 621 896 990

Pages