Breaking

Thursday, 16 May 2024

MAKONDA AIPONGEZA BENKI YA CRDB MSAADA WA PIKIPIKI KWA JESHI LA POLISI KUIMARISHA USALAMA KWA WATALII JIJINI ARUSHA

 

Arusha 16 Mei 2024 - Serikali imeipongeza Benki ya CRDB kwa kutoa msaada wa pikipiki kwa Jeshi la Polisi mkoani Arusha ili kuimarisha doria zitakazoongeza usalama kwa watalii wanaokuja nchini. Pongezi hizo zimetolewa na Mkuu wa Mkoa wa Arusha, Paul Makonda alipopokea pikipiki hizo zenye thamani ya Shilingi Milioni 50 kwenye hafla fupi ya makabidhiano iliyofanyika katika Hoteli ya Gran Melia ya jijini humo.

Makonda amesema sekta ya utalii ina umuhimu mkubwa katika uchumi na maendeleo ya wananchi nchini kwani ndiyo inayoongoza kwa kuliingizia taifa fedha nyingi za kigeni, ikiwa ya pili kwa kuchangia kwenye Pato la Taifa, na ya tatu kwa kutoa ajira.
“Nitoe shukrani zangu za dhati kwa msaada huu wa pikipiki 20 ambao Benki ya CRDB imeutoa kwa Jeshi letu la Polisi. Pikipiki hizi zitasaidia askari wetu kutekeleza majukumu yao kwa ufanisi na hivyo kuimarisha usalama kwa watalii na kuufanya mkoa wetu kuwa kivutio kikubwa cha wageni,” amesema Makonda huku akipongeza pia mpango wa Benki hiyo kuwawezesha wananchi kujenga nyumba za malazi maarufu kama ‘BNB’ kupitia programu ya IMBEJU inayotekelezwa na taasisi yake ya CRDB Bank Foundation.

Mwaka 2020, sekta ya utalii ilichangia asilimia 10.6 kwenye pato la taifa ila kiasi hichi kilishuka hadi asilimia 5.7 mwaka 2021 kutokana na athari za UVIKO-19 hivyo kuilazimu Serikali kuchukua hatua za makusudi kuifufua kwa kufuata taratibu za Shirika la Afya Duniani (WHO) na kufanya matangazo kimataifa kwa Rais Samia Suluhu Hassan mwenyewe kurekodi filamu ya ‘The Royal Tour.’
Mwaka 2023, idadi ya watalii waliofika Tanzania iliongezeka kwa asilimia 24.3 hadi kufikia 1,808,205 kulinganisha na watalii 1,454,920 mwaka 2022. Mapato ya utalii ya Tanzania yalifikia rekodi ya juu ya Dola za Marekani 3,368.7 milioni ikilinganishwa na Dola za Marekani 2,527.8 milioni mwaka 2022. Kutokana na kuimarika kwa sekta hiyo, Baraza la Taifa la Biashara (TNBC) limekadiria kuwa katika mwaka wa fedha 2025/2026 sekta ya utalii itachangia 19.5% ya Pato la Taifa.

Ili kuhakikisha usalama wa watalii wanaokuja nchini, Serikali ilianzisha kitengo maalum cha utalii na diplomasia kwa ajili ya kuwahudumia watalii na wanadiplomasia wanaofika nchini kutalii ama kuwekeza kwa haraka. Kwa kuwa jiji la Arusha ndio kitovu cha utalii nchini, kituo hicho kimejengwa huko na askari wake walipewa mafunzo ya ziada ndani na nje ya nchi.
Akikabidhi pikipiki hizo, Mkurugenzi Mtendaji wa Benki ya CRDB, Abdulmajid Nsekela amesema kila mmoja anafahamu umuhimu wa amani, utulivu na usalama katika maendeleo ya nchi kiuchumi, kijamii na kisiasa hivyo Benki hiyo imetoa kipaumbele katika eneo hilo kupitia Sera yake ya Uwekezaji katika Jamii.

“Pamoja na kuwepo hali ya amani na utulivu nchini, bado baadhi ya matukio ya uhalifu hujitokeza kama vile vile uporaji wanaofanyiwa raia hata watalii wanaokuja kutembelea vivutio vilivyopo nchini. Ili Jeshi la Polisi litekeleze majukumu yake kwa ufanisi linahitaji vitendea kazi vya kutosha,” amesema Nsekela.
Mkurugenzi huyo amesema pikipiki hizo zitakwenda kuwasaidia askari kuwadhibiti wahalifu wanaowapora watalii na wananchi wengine hivyo kuharibu sifa njema za jiji hilo la kitalii. Mwaka jana Benki ya CRDB ilikabidhi pikipiki 15 kwa ajili ya kituo hicho kwa aliyekuwa Waziri wa Utalii wa kipindi hicho, Mohammed Mchengerwa.
Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia langolahabari@gmail.com au WhatsaApp: +255 621 896 990

Pages