Breaking

Monday, 27 May 2024

MAKAMU MWENYEKITI WA CCM TAIFA AKABIDHI MITUNGI YA ORYX KWA WANANCHI WA JIMBO LA MOROGORO KUSINI MASHARIKI

Na Mwandishi Wetu, Ngerengere

MAKAMU Mwenyekiti wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) Tanzania Bara Abdulurhaman Kinana amesema kampeni ya nishati safi iliyoanzishwa na Rais Dk. Samia Suluhu Hassan inalenga kumtua mwanamke mzigo wa kuni kichwani na kumpa muda mwingi wa kujikita katika shughuli za maendeleo.

Akizungumza wilayani Morogoro Vijijini wakati Mbunge wa Jimbo la Morogoro Kusini Mashariki Hamis Taletale kwa kushirikiana na Kampuni ya Oryx Gas Tanzania wakikabidhi mitungi ya gesi 800 yakiwa na majiko yake kwa wananchi,Kinana amesema uamuzi huo unakusudia kusaidia kuwainua wananchi na hasa wanawake.

Katika tukio hilo ambalo limekwenda sambamba na Mbunge wa Jimbo hilo kutoa taarifa ya utekelezaji wa Ilani ya Uchaguzi Mkuu katika kipindi cha miaka mitatu,Kinana ameeleza kwa kuhusu dhamira ya Rais Samia katika kuhamasisha nishati safi ya kupikia.

“Leo nitaikabidhi mitungi ya gesi kwa wananchi,nampongeza Taletale pamoja na wadau hawa wa gesi .Uwepo wa mitungi hii ni matokeo ya sera na ubunifu wa Rais Dk. Samia Suluhu Hassan.Alianzisha mchakato wa kuwatua akina mama mzigo wa kuni, kaanzisha mradi wa nishati safi na salama.

“Mwaka jana lilifanyika kongamano kubwa, lakini Rais akaona shughuli hii inahitaji fedha nyingi sana, inahitaji kuungwa mkono na dunia nzima, inahitaji msaada wa watu wenye uwezo, Rais si msemaji sana lakini ni mtendaji wa hali ya juu. 

"Hivi karibuni alikuwa Ufaransa katika mkutano wa nishati safi ambao alikuwa Mwenyekiti Mwenza uliolenga kuasidia kumtua mama mzigo wa kuni.Kuna maelfu ya akina mama wanafariki dunia kwa sababu ya matumizi ya kuni na mkaa, Rais Dk. Samia ameamua kuanza kampeni ya kuhakikisha kila nyumba inatumia gesi ya kupika.

“Nchi yetu ina umri wa miaka 60 jambo hili halijawahi kufikiriwa wala kubuniwa, lakini Rais Samia ameona umuhimu wake, inawezekana anawajali sana Watanzania lakini ni ukweli usiopingika anawajali sana akina mama, ndio maana amelichulikua jambo hili kwa uzito wake,"amesema Kinana.

Kwa upande wake Meneja wa Mifumo ya Gesi yenye Matumizi Makubwa Oryx Gas Tanzania LTD, Richard Sawere aliyezungumza kwa niaba ya Mkurugenzi Mkuu wa Kampuni ya Gesi ya Oryx Tanzania, Benoite Araman, amesema ugawaji wa mitungi hiyo ni kuunga mkono jitihada za Rais Dk. Samia ambaye amedhamiria ifikapo mwaka 2030 asilimia 80 ya Watanzania wawe wananatumia nishati safi ya kupikia.

Amesema Kampuni ya Oryx imegawa mitungi na majiko hayo ya gesi kunusuru uharibifu wa mazingira na kulinda afya za wananchi kwa kutumia nishati safi na rafiki kwa afya za wananchi.

"Nchini Tanzania, wananchi 33,000) wanapoteza maisha kila mwaka kwa kuvuta moshi na chembe chembe zinazotokana na mkaa na kuni. Kupika na gesi ya Oryx itatatua jambo hili," amesema na kuongeza nia ya Oryx ni kuhakikisha Watanzania wote wanaachana na matumizi ya kuni na mkaa wataki wa kupika.

Awali Mbunge wa Jimbo la Morogoro Kusini Mashariki Hamis Taletale amesema kuwa anaishukuru Kampuni ya Oryx kwa kushirikiana naye katika kufanikisha ugawaji bure wa mitungi hiyo ya gesi kwa wananchi zaidi ya 880 na lengo ni kumuunga mkono Rais Samia Suluhu Hassan ambaye amekuwa akihamasisha na kuelekea utekelezaji wa matumizi ya nishati safi ya kupikia.










Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia langolahabari@gmail.com au WhatsaApp: +255 621 896 990

Pages