Breaking

Tuesday 28 May 2024

KLABU ZA MAZINGIRA DAWASA ZAJIFUNZA UTUNZAJI MAZINGIRA, UZALISHAJI MAJI

Mamlaka ya Majisafi na Usafi wa Mazingira Dar es salaam (DAWASA) imeratibu ziara ya mafunzo kwa wanafunzi wa sekondari Saranga na shule ya Msingi Mkuranga kutembelea Mtambo wa uzalishaji Maji Ruvu Juu na chanzo cha Maji Kulungu kilichopo Mkuranga ikiwa ni lengo la kuwajengea uelewa juu ya utunzaji Rasilimali maji na uhifadhi wa vyanzo vya maji.

Akizungumza katika ziara hiyo Ndugu Husna Richard, Afisa mawasiliano DAWASA amesema kuwa Mamlaka inatambua umuhimu wa kutengeneza kizazi kijacho kinachotambua na kuthamini umuhimu wa huduma ya maji pamoja na utunzaji wa miundombinu ya maji na hivyo ziara za mafunzo ni muhimu sana kwa wananfunzi hao.

"Tumefanya ziara nzuri ya mafunzo kutoka kwa Wananfunzi wa Shule za Saranga na Mkuranga ambazo ni baadhi ya shule zenye klabu za Mazingira zinazosimamiwa na DAWASA, kupitia mafunzo haya wamepata nafasi ya kutembelea na kujifunza juu ya shughuli zinazofanywa na DAWASA katika uzalishaji na usambazaji wa Maji pamoja na jitihada zinazofanywa katika kulinda vyanzo vyetu vya maji. Huu ni muendelezo wa mafunzo tutakayoendelea kutoa katika shule zilizo ndani ya eneo letu la kihuduma.

Kupitia mafunzo haya pia Wanafunzi walipata nafasi ya kushiriki zoezi la upandaji miti katika chanzo cha Maji Kulungu kinachosaidia kuzalisha maji kwa Wakazi wa Mkuranga na kuongeza hamasa kwa wanafunzi kutunza na kusimamia uhifadhi wa mazingira.

Mwalimu mlezi wa klabu ya mazingira kutoka shule ya sekondari Saranga, ndugu Aidan Mwangalimi ameishukuru Mamlaka kwa kutoa nafasi kwa wanafunzi kujifunza na kujionea kwani imekuwa chachu kwa wanafunzi kutamani kuwa wataalamu wa maswala mbalimbali yanayohusiana na maji na usafi wa mazingira.

Mamlaka ya Majisafi na Usafi wa Mazingira Dar es salaam (DAWASA) ni mlezi wa klabu za Mazingira 12 zilizopo katika shule za Sekondari na Msingi Mkoani Dar es salaam na Mkoa wa Pwani.







Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia langolahabari@gmail.com au WhatsaApp: +255 621 896 990

Pages