Breaking

Monday, 22 April 2024

TANZANIA YAONGOZA KWA SIMBA, NYATI NA CHUI BARANI AFRIKA


Na John Mapepele

Serikali imesema Tanzania inaongoza kwa kuwa na Simba, Nyati na Chui wengi katika bara la Afrika huku ikishirikilia nafasi ya tatu kwa kuwa na idadi kubwa yaTembo.

Hayo yamesemwa leo Aprili 22, 2024 kwenye mkutano ambao Waziri wa Maliasili na Utalii, Mhe. Angellah Kairuki ametangaza rasmi matokeo ya Sensa ya Wanyamapori na kuzindua taarifa ya Watalii wa Kimataifa walioitembelea Tanzania mwaka 2023.

Sensa hiyo ya wanyamapori imefanywa na TAWIRI kwa kushirikiana na TANAPA, TAWA, NCAA, Idara ya Wanyamapori, na Frankfurt Zoological Society katika mifumo ya ikolojia ya Nyerere-Selous-Mikumi,Saadani-Wamimbiki na Serengeti 

Mkutano huo uliwahusisha wadau wa uhifadhi na utalii, ambapo Mhe. Kairuki amesema tayari Serikali imetenga fedha kwa ajili ya kufanya sensa ya wanyamapori nchi nzima mapema hapo mwakani.

 Aidha, Mhe. Kairuki amesema matokeo ya sensa hiyo yatasaidia kwenye usimamizi wa wanyamapori nchini na kupanga mipango mbalimbali ya kuboresha  uhifadhi na  kutangaza  utalii duniani.

Mhe. Kairuki ametoa wito kwa wadau wote kushirikiana na Serikali ambapo ameitaka Taasisi ya Utafiti wa Wanyamapori nchini (TAWIRI) kuandaa mpango kazi kwa ajili ya sensa ijayo huku pia akielekeza watendaji wa wizara yake kuchambua kwa kina  matokeo ya sensa hii  ili yaweze kuleta tija.
.

Akitoa taarifa ya sensa hiyo amesema spishi zilizoonyesha idadi kubwa ni pamoja na Nyati (59,878), Tembo (20,006), Nyumbu (19,060), Kongoni (18,361), swalapala (14,031) na Ngiri (13,806), ambapo spishi zilizoonyesha idadi ndogo ni pamoja na Twiga (1,679), Tandala mkubwa/ kudu (1,414) na puku/sheshe (496). 

Amefafanua kuwa kwa upande wa Tembo, idadi imeongezeka kutoka 15,501 (2018) hadi 20,006 (2022) na Viashiria vya ujangili wa tembo au vifo vya tembo vimepungua kwa kiasi kikubwa hadi 0.8% mwaka 2022 ikilinganishwa na 16% wakati wa sensa ya 2018. 

Akizungumzia kuhusu taarifa ya Watalii wa Kimataifa walioitembelea Tanzania mwaka 2023 amesema Sekta ya Utalii ni miongoni mwa sekta muhimu katika uchumi wa dunia na umeendelea kuimarika baada kuathiriwa na mlipuko wa janga la UVIKO-19. Mwaka 2023 sekta ya utalii duniani imeimarika kwa kiwango cha asilimia 88 ikilinganishwa na kiwango cha juu kilichofikiwa mwaka 2019.

 “Hali hii ilitokana na ukuaji endelevu wa maendeleo ya teknolojia na juhudi za kukuza na kuendeleza maeneo mengine ya utalii duniani. Takwimu zinaonyesha kuwa idadi ya watalii duniani iliongezeka kwa asilimia 34 hadi kufikia watalii bilioni 1.3 Mwaka 2023 kutoka milioni 960 Mwaka 2022”. Ameongeza

Amesema kwa Tanzania, utalii wa Kimataifa umeimarika kwa kiwango cha asilimia 118.4 Mwaka 2023 ikilinganishwa na kiwango cha juu kabla ya janga la UVIKO-19.  Aidha, idadi ya watalii wa Kimataifa iliongezeka kutoka watalii milioni 1.4 Mwaka 2022 hadi kufikia watalii milioni 1.8 Mwaka 2023 sawa na ongezeko la asilimia 24.3. 

“Hatuna budi kutambua kazi kubwa aliyoifanya Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan, Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania aliyeitangaza Tanzania kupitia filamu ya Tanzania the Royal tour”. Amesisitiza  

Kwa kutambua umuhimu wa sekta ya utalii hapa Nchini, Serikali kwa kushirikiana na wadau ilifanya utafiti wa watalii wanaoondoka Nchini Mwaka 2023 kwa lengo la kupata taarifa zinazosaidia kutunga Sera na kuandaa mipango ya maendeleo ya utalii. Aidha, taarifa za utafiti huo zinasaidia serikali kuandaa akaunti za taifa (national accounts) na mizania ya malipo ya nje (Balance of Payments). 

Aidha amesema utafiti umebainisha kuwa mapato yatokanayo na utalii yaliongezeka kwa asilimia 33.5 hadi kufikia Dola za Marekani bilioni 3.4 Mwaka 2023 kutoka Dola za Marekani 2.5 bilioni zilizopatikana Mwaka 2022.  Aidha, wastani wa matumizi ya mtalii kwa siku katika Jamhuri ya Muungano wa Tanzania uliongezeka hadi kufikia Dola za Marekani 250 Mwaka 2023 kutoka wastani wa Dola za Marekani 214 Mwaka 2022. 

Kwa upande wa Zanzibar, wastani wa matumizi ya mtalii kwa siku ulikuwa Dola za Marekani 257 Mwaka 2023 ikilinganishwa na watani wa Dola za Marekani 218 Mwaka 2022.
Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia langolahabari@gmail.com au WhatsaApp: +255 621 896 990

Pages