Breaking

Friday, 12 April 2024

PROF. GURNAH AWASILI NCHINI, KUSHIRIKI UTOAJI TUZO YA UANDISHI BUNIFU APRILI 13,2024

NA EMMANUEL MBATILO, DAR ES SALAAM

MGENI rasmi katika hafla ya utoaji tuzo ya Taifa ya Mwalimu ya uandishi bunifu, Prof.Abdulrazak Gurnah amewasili nchini leo April 12,2024 akipokelewa na mwenyeji wake Waziri wa Elimu Prof..Adolf Mkenda akiwa ameambatana na Mkurugenzi Mkuu wa Taasisi ya Elimu Tanzania (TET) Dkt.Aneth Komba.

Akizungumza na waandishi wa habari leo April 12 2024,Jijini Dar es Salaam Waziri wa Elimu Dkt.Adolf Mkenda ameonesha furaha yake wakati akimpokea mgeni huyo ambaye atashiriki zoezi la utoaji tuzo.

Prof.Mkenda amempongeza Prof.Gurnah kwa ukubali wake wa kuja kuwa mgeni rasmi katika zoezi la utoaji tuzo ya Taifa ya Mwalimu Nyerere ya uandishi bunifu itakayofanyika katika ukumbi wa The Super Dome Masaki Jijini Dar es Salaam.

Kwa Upande wake Prof.Abdulrazak Gurnah ameishukuru serikali kumpatia heshima kubwa ya kuja kuwasaidia waandishi wanaopatikana nchini ikiwa kuwapatia uzoefu wake alionao kwa lengo la kuinua tasnia ya uandishi bunifu.

Aidha Prof.Gurnah amesema kuwa hafikirii matumizi ya akili bandia (artificial intelligence) yataathiri kukua kwa waandishi bunifu kwa sababu andiko la mwandishi linatoa sauti (wazo) moja kwa moja tofauti na matumizi ya akili bandia ambayo hayatoi kitu halisi.

Pamoja na hayo Prof.Gurnah ameeleza kuwa ili kuongezeka kwa waandishi wengi wa fasihi na uandishi bunifu watu wengi wanapaswa kusoma ndipo watahamasika kuandika waliyonayo.

Prof.Gurnah ambaye ni mwandishi mkongwe na Mkufunzi katika Chuo cha Kent kinachopatikana nchini Ungereza alitunukiwa tuzo ya Nobel 2021 kwa uandishi wake bora wa fasihi kwa kuchunguza athari za ukoloni katika utambulisho wa Afrika Mashariki, na uzoefu wa wakimbizi wanapolazimika kutafuta makazi kwingine.

Tuzo hiyo ya Taifa ya Mwalimu Nyerere ambayo imeletwa mahususi kwaajili ya kumuenzi Baba wa Taifa na Rais wa kwanza wa Tanzania inatarijiwa kutolewa kesho April 13,2024 katika vipengele vya Riwaya,Ushahiri na hadithi za watoto.
Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia langolahabari@gmail.com au WhatsaApp: +255 621 896 990

Pages