Breaking

Saturday, 13 April 2024

NAIBU WAZIRI PINDA AOMBA UCHUNGUZI FEDHA ZA WMA MPIMBWE

Na Munir Shemweta, MLELE

Mbunge wa Jimbo la Kavuu na Naibu Waziri wa Ardhi Nyumba na Maendeleo ya Makazi Mhe. Geophrey Pinda amemuomba Mkuu wa wilaya ya Mlele mkoa wa Katavi Alhaji Majid Mwanga kuunda Tume ya Kupitia Mapato na Matumizi ya fedha za Jumuiya ya Hifadhi ya Wanyamapori (WMA) katika halmashauri ya Mpimbwe ili kubaini kama kuna ubadhilifu basi wahusika wachukuliwe hatua kali.

Aidha, amemuomba mkuu huyo wa wilaya ya Mlele kuchunguza kiasi cha fedha milioni 44 kilichotolewa na Mkandarasi anayejenga barabara ya Kibaoni hadi Sitalike zinazodaiwa kulipwa kwa kijiji bila kufuata utaratibu.

Mhe. Pinda ametoa kauli hiyo kwa nyakati tofauti tarehe 12 April 2024 wakati wa mikutano yake ya hadhara na wananchi wa vijiji vya Mirumba, Ilalangulu na Kibaoni katika halmashauri ya Mpimbwe wilaya ya Mlele mkoa wa Katavi.

Kauli Mhe. Pinda inakuja mara baada ya kubadilishwa uongozi wa Kamati ya Kusimamia WMA ndani ya mwezi mmoja tu kamati ilifanikiwa kukusanya shilingi milioni 200 tofauti na kamati iliyokaa kwa zaidi ya miaka kumi na kudaiwa kutosaidia maendeleo yoyote ya vijiji husika.

"Iundwe tume ya kupita kitabu kwa kitabu tujue miaka 20 fedha zetu zilienda wapi za wananchi hao, wiki mbili milioni 200 hebu tuwaulize miaka 20 wameleta nini?" Alihoji Mhe. Pinda.

"Pia kuna ubadhilifu wa milioni 44 zilizotolewa na mkandarasi anayejenga barabara ya kiabaoni- Sitalike ambaye amelipa fedha kwa kijiji bila utaratibu. Uchunguzi nani amechukua fedha taslimu ambazo hazijulikani zilipokwenda wapi ufanyike". Amesema Mhe. Pinda.

Aidha, ameuelezea mpango wa WMA kama wenye faida kubwa kwa vijjji vinavozunguka hifadhi na kutolea mfano wa wilaya ya Tanganyika kama wilaya inayonufaika na mpango huo ambapo kwa mujibu wa Mhe. Pinda mwaka huu wa 2024 vijiji vinavyozunguka hifadhi vinaenda kupokea shilingi bilioni 16 .

Amesema kuwa, kiasi chochote cha fedha kitakachopatikana kupitia mpango wa WMA lazima wananchi wahusishwe matumizi yake ili fedha zinazokusanywa ziende kutumika kwenye shughuli za maendeleo ya vijiji husika.

Mkuu wa wilaya ya Mlele mkoa wa Katavi Alhaji Majid Mwanga ameahidi kuunda haraka Tume itakayohusisha vyombo vya ulinzi na usalama kama vile TAKUKURU, Jeshi la Polisi na Magereza ili kubaini kama upo ubadhilifu wowote wa fedha za umma basi wahusika waweze kuchukuliwa hatua stahiki.

"Hakuna atakayepona katika suala hilo na lazima tutawashughulikia wahusika wote waliowaibia wananchi. Kazi hii tunaiweza na hatutacheka na mtu hata mmoja". Amesema Alhaji Mwanga.

Jumuiya ya Hifadhi ya Wanyamapori ya Jamii (WMA) katika halmashauri ya Mpimbwe wilaya ya Mlele inahusisha vijiji vya Kibaoni, Mirumba, IIalangula pamoja na kijiji kimoja kutoka wilaya ya Nkasi.
Mbunge wa jimbo la Kavuu na Naibu Waziri wa Ardhi Nyumba na Maendeleo ya Makazi Mhe. Geophrey Pinda akizungumza na wananchi wa Kata ya Kibaoni wakati wa ziara yake ya kuzungumza na wananchi tarehe 12 April 2024.
Mkuu wa wilaya ya Mlele mkoa wa Katavi Alhaji Majid Mwanga akizungumza wakati wa ziara ya Mbunge wa Jimbo la Kavuu na Naibu Waziri wa Ardhi Nyumba na Maendeleo ya Makazi Mhe. Geophrey Pinda katika kijiji cha Mirumba halmashauri ya Mpimbwe mkoa wa Katavi tarehe 12 April 2024.
Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri ya Mpimbwe Bi. Shamim Daud Mwariko akizungumza katika ziara ya Mbunge wa Jimbo la Kavuu na Naibu Waziri wa Ardhi Nyumba na Maendeleo ya Makazi Mhe. Geophrey Pinda katika jimbo la Kavuu  tarehe 12 April 2024.
Mbunge wa jimbo la Kavuu na Naibu Waziri wa Ardhi Nyumba na Maendeleo ya Makazi Mhe. Geophrey Pinda akisisitiza jambo wakati akizungumza na wananchi wa Kata ya Ilalangulu kwenye halmashauri ya Mpimbwe mkoa wa Katavi wakati wa ziara yake ya kuzungumza na wananchi tarehe 12 April 2024.
Baadhi ya wananchi wa kijiji cha Ilalangulu katika halmashauri ya Mpimbwe mkoa wa Katavi wakimsikiliza Mbunge wa Jimbo la Kavuu na Naibu Waziri wa Ardhi Nyumba na Maendeleo ya Makazki Mhe. Geophrey Pinda (hayupo pichani) wakati wa ziara yake ya kuzungumza na wananchj tarehe 12 April 2024. (PICHA ZOTE NA WIZARA YA ARDHI)
Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia langolahabari@gmail.com au WhatsaApp: +255 621 896 990

Pages