Breaking

Sunday, 7 April 2024

MTANZANIA MASHUHURI MITANDANI DOTTO MAGARI AWEKEZA MIL 70 KIJIJI CHA NGURUWE BAHI DODOMA

 

 
DODOMA . Mtu mashuhuri na Mwenye ushawishi mkubwa Mitandaoni Dotto Ketto maarufu Dotto Magari amefanya uwekezaji mkubwa wa nguruwe wenye thamani ya shilingi milioni 70 katika kijiji cha Nguruwe katika kitongoji cha Namahero kijiji cha Mayamaya wilayani Bahi mkoani Dodoma na kisha kuwataka vijana kuacha tabia ya kushinda mitandaoni bila sababu za msingi na badala yake waingie kwenye uwekezaji wa mifugo na hata kilimo.

Dotto Magari amesema miezi michache iliyopita alifika katika mradi wa Nguruwe katika kijiji cha Nguruwe kwa lengo la kujifunza uendeshaji na mazingira ya mradi huo na kisha kuamua kuwekeza fedha baada ya kuridhishwa na utekelezaji wake.

Amesema ameshangazwa kuona nguruwe wanaokaribia elfu moja wakati miezi minne iliyopita kulikuwa na nguruwe wachache tu hivyo wakati umefika kwa yeyote aliyethubutu kuungana naye kuwekeza katika ufugaji wa nguruwe katika kijiji cha Nguruwe Bahi kwa sababu miezi sita ijayo anategemea kupata zaidi ya mil 200 kwenye uwekezaji wa shilingi milioni 70.

"Nimeridhishwa na mazingira ya uwekezaji naamini hakuna ujanja ujanja na unatakiwa kujua mimi ni muislamu lakini linapokuja suala la uwekezaji biashara yeyote anaweza kuifanya kwa namna mbalimbali na kisha kuwapiga vijembe watu mashuhuri mitandaoni wanaotumia umaarufu wao kuchafuana tu",amesema Dotto Magari.

Awali akiweka bayana mpango wa mradi huo mwanzilishi wa kijiji cha Nguruwe ambaye pia ni mkurugenzi wa Nguruwe Project Simon Mkondya amesema kusudio lake ni kulifanya eneo hilo kuwa mzalishaji mkubwa wa nguruwe kwa sababu mahitaji ya kitoweo chake yamezidi kukua kwa kasi hapa nchini na Afrika kwa Ujumla.
Mkondya amesema mpango mwingine uliopo ni kwamba ifikapo julai mwaka huu wanakwenda kujenga kiwanda cha kuchakata nyama ya nguruwe ambayo itakuwa ikiuzwa ndani na nje ya nchi na kisha viungo vingine kugawa bure kwa makundi yenye uhitaji kama vile watoto yatima ,Wajawazito na wazee ili kurejesha kwa jamii.

Kuhusu Suala la Soko mwanzilishi huyo wa kijiji cha Nguruwe amesema nchi ya Uholanzi ina uhitaji wa nguruwe elfu tano kila wiki huku wateja wakubwa wa ndani wakizidi kuongezeka kila kukicha wakiwemo wadada wakidai huenda inasaidia kuongeza mwonekano wao.

"Nguruwe mmoja mwenye mimba ni sawa na Ng'ombe mia tano baada ya miaka miwili kwa sababu katika kipindi hicho nguruwe mmoja atazaa watoto 160 huku uzazi wao wa kwanza nao ukiwa tayari umeanza kuzaa hivyo kila mtu aitazame fursa hii kwa jicho la tofauti", amesema Mkondya.

Kwa upande wake mwenyekiti wa kitongoji cha Zamahero Wilson Mazinya ametoa shukrani na kisha kuahidi kumpa ushirikiano muasisi wa mradi huo ambao umetoa ajira kwa vijana zaidi ya 70 na kuinua biashara zao kutokana na kupata fedha za kitalii kutoka ndani na nje ya Tanzania huku mmoja kati ya vijana waliyonufaika na ajira akiwemo Aman Marcel akisema amejenga kibanda na kuendesha familia kupitia mradi huo.
Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia langolahabari@gmail.com au WhatsaApp: +255 621 896 990

Pages