Breaking

Wednesday, 24 April 2024

MADEREVA BODABODA DODOMA WAISHUKURU AMENDA KWA KUWAPATIA MAFUNZO USALAMA BARABARANI

Na Mean Wetu,Dodoma

MADEREVA bodaboda katika Jiji la Dodoma wameeleza jinsi mafunzo ya elimu ya usalama barabarani yalivyo wafumbua macho na kuwafanya kufahamu sheria mbalimbali za barabarani na hivyo kuendelea na kazi yao wakiwa salama.

Wamesema hayo mbele ya waandishi wa habari waliokuwa wametembelea kijiwe cha bodaboda cha Kijiwe Pesa ambapo baadhi ya bodaboda walikuwa wakifanya tathimini kuhusu mafunzo waliyopata kutoka Amend kwa ufadhili wa Ubalozi wa Uswisi ambao wameendelea kufanikisha kutolewa kwa mafunzo hayo.

Madereva hao bodaboda katika kijiwe hicho wamesema awali hawakuwa wakifahamu vema sheria za usalama barabarani hasa taa zinazoongoza magari na jinsi ya kupita kwenye makutano ya barabara ilikuwa ni kitendawili kwao.

"Kupitia mafunzo ya usalama barabarani ambayo tumeyapata kutoka kwa wenzetu wa Amend kwa kushirikiana na wadau wengine kama Jeshi la Polisi Kikosi cha Usalama barabarani sasa tunafahamu vema sheria za usalama barabarani pamoja na alama zilizopo,"amesema dereva bodaboda Jonathan Chidawi

Kwa upande wake Amiri Matimba ambaye ni Msaidizi wa Miradi kutoka Shirika la Amend Tanzania anasema wamefanikiwa kutoa mafunzo kwa madereva bodaboda 47 kwa wiki ya kwanza jijini Dodoma.

Ameongeza kuwa wanaendelea kutembea katika vijiwe mbalimbali vya bodaboda kwa ajili ya kuhamasisha maofisa hao kusafirishaji(bodaboda)kujiunga katika mafunzo hayo yanayotolewa bila gharama yoyote.

Wakati huo huo Mkufunzi wa Mafunzo hayo ambae pia ni Katibu wa Chama cha Walimu wa madereva Tanzania (CHAWATA) Massava Ponera akieleza tathimi ya mafunzo hayo toka walipoanza hadi walipofikia amesema mafunzo yanaendelea na madereva wengi wamefikiwa na mafunzo hayo.

Amefafanua kwa Dodoma hiyo ni awamu ya pili kutolewa kwa mafunzo hayo ambayo yamedhaminiwa na ubalozi wa Uswisi ili kuwezesha elimu ya usalama barabarani inafika kwa kundi la bodaboda ambalo jamii siku zote hulitazama kwa jicho la tofauti na kuamini ni wavunjaji wa sheria wakubwa.
Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia langolahabari@gmail.com au WhatsaApp: +255 621 896 990

Pages