Mamlaka ya Majisafi na Usafi wa Mazingira Dar es Salaam (DAWASA) imeendelea kutoa elimu katika klabu za maji na usafi wa Mazingira kwa katika shule ya sekondari Saranga iliyopo Wilaya ya Ubungo na kusisitiza juu ya uhifadhi wa mazingira kwa uhakika wa huduma za Maji.
Shule hiyo ni miongoni mwa shule 11 za Mazingira zinazosimamiwa na kuendeshwa na Mamlaka ya Majisafi na Usafi wa Mazingira (DAWASA).
Afisa Mawasiliano kutoka DAWASA Bi Husna Richard ameeleza njia mbalimbali za utunzaji wa vyanzo vya Maji na kusisitiza umuhimu wa utunzaji wa Mazingira katika kuhakikisha upatikanaji wa majisafi kwa wote.
“Huduma ya majisafi inategemea sana ulinzi wa vyanzo vya Maji na uwepo wa miti rafiki ya mazingira, hivyo ili kuhakikisha tunaendelea kunufaika na huduma ya maji ni wajibu wa kila mmoja kutunza mazingira kwa kupanda miti katika maeneo tunayoishi” amesema Ndugu Husna.
Nae Mwalimu Bupe Asajile mlezi wa klabu ya mazingira shuleni hapo ameishukuru Mamlaka kwa jitihada za kutoa elimu ya usafi wa mazingira na ulinzi wa vyanzo vya maji kwa wanafunzi.
“Elimu ya utunzaji wa mazingira na ulinzi wa vyanzo vya maji ni elimu inayopaswa kurithishwa kwa watu wa rika zote, kuanza na hawa wanafunzi wadogo kunawasaidia kujijengea tabia endelevu na kuchukua majukumu ya utunzaji wa mazingira. Kuelimisha vijana ni adhina ya kudumu,” amesema Mwl. Bupe.
Nae mwanafunzi Maximillian Kavishe ambae ni mwanachama wa klabu ya maji na usafi wa mazingira ya shule ya Sekondari Saranga ameishukuru Mamlaka kwa kuwa mlezi na kutoa nafasi ya wao kujifunza mambo mbalimbali ya Maji na Usafi wa Mazingira na kuomba nafasi ya kuendelea kujifunza kwa vitendo ili kufahamu zaidi namna Mamlaka inavyoendesha shughuli zake.
Mamlaka inakusudia kuelimisha vijana kuhusu utunzaji wa mazingira ili wajenge uwezo na uelewa mkubwa wa maswala ya maji na usafi wa Mazingira, pia imejikita katika kuhakikisha inafikia wanajamii wa rika zote na kutoa elimu, kwani inaamini mabadilko ya kitabia yatachangia kuwepo kwa utamaduni mzuri wa uhifadhi wa mazingira na kudumu kwa miundombinu ya majisafi na majitaka, wanafunzi ni mabalozi wazuri katika jamii.
Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia langolahabari@gmail.com au WhatsaApp: +255 621 896 990
Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia langolahabari@gmail.com au WhatsaApp: + 255 621 615 613 au +255 621 896 990