Breaking

Sunday, 17 March 2024

WANANCHI ELFU 9,659 KUNUFAIKA NA MRADI WA MAJI MALUNGU NYASA

NAIBU Waziri wa Maji Mhandisi Maryprisca Mahundi amemuagiza Meneja wa RUWASA Mkoa wa Ruvuma Mhandisi Rebman Ganshonga, kuhakikisha anapeleka huduma ya maji kwenye vitongoji ambavyo bado havina huduma ya maji.

Mhandisi Mahundi ametoa maagizo hayo leo Machi 17, 2024 akiwa katika muendelezo wa ziara ya kamati ya Kudumu ya Bunge ya Maji na Mazingira ya kukagua utekelezaji wa miradi ya Maji Mkoani Ruvuma

Akiwa ziarani pia Mhandisi Mahundi ametoa rai kwa wananchi kuendelea kutunza vyanzo vya maji ili miradi ya maji iwe endelevu.

Nae Mwenyekiti wa Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Maji na Mazingira Mhe.Jackson Kiswaga ameishukuru Serikali kupitia Wizara ya Maji kwa usimamizi na utekelezaji wa miradi.

"Mradi huu ukamilike kwa wakati pia wananchi muweze kutunza Miundombinu yake ili mradi uwe endelevu. Lakini chombo cha watumiaji maji katika jamii kiundwe ili kiweze kukusanya fedha na kufanya matumizi mazuri ya ukarabati wa mradi pindi inapotokea mradi umeharibika"amesema Mhe.Kiswaga

Akitoa taarifa ya utekelezaji wa mradi wa maji Malungu Meneja wa RUWASA Wilaya ya Nyasa Mhandisi Masoud Samila amesema mradi wa Malungu unatekelezwa kwa gharama ya Shilingi Bilioni 1.2

Mhandisi Samila amesema kukamilika kwa mradi huo kunalenga kuwanufaisha wananchi wapatao 9,659 kutoka vijiji vya Malungu na Tingi vilivyopo katika kata ya Tingi.

" Mradi pia utasaidia kupunguza magonjwa mbalimbali ya mlipuko kwa jamii. Vilevile kutokana na kuimarika kwa huduma ya maji, jamii itapata muda wa kufanya shughuli za maendeleo"amesema Mhandisi Samila
Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia langolahabari@gmail.com au WhatsaApp: +255 621 896 990

Pages