Na Mwandishi Wetu
Diwani wa Kata ya Songo Songo, Mkoani Lindi, Mhe. Hassan Swalehe Yusuph ameipongeza Mamlaka ya Udhibiti Mkondo wa Juu wa Petroli (PURA) kwa usimamizi bora wa Miradi ya Uwajibikaji kwa Jamii (CSR) iliyofanywa na kampuni zinazozalisha gesi asilia katika kisiwa cha Songo Songo.
Mhe. Yusuph ametoa pongezi hizo hivi karibuni wakati akizungumza na wataalamu wa PURA waliombatana na wadau wa vyombo vya habari walipofanya ziara kisiwani humo kwa lengo la kutembelea miradi hiyo ambayo inatekelezwa na Shirika la Maendeleo ya Petroli (TPDC) na Kampuni ya PanAfrican Energy Tanzania (PAET).
“PURA imefanya kazi kubwa ya kuja na Miongozo Juu ya Uwajibikaji wa Makampuni kwa Jamii itakayotoa namna bora ya utekelezwaji wa miradi hii jambo ambalo limekuwa chachu kwa wananchi kupata miradi wanayoitaka na inayoendana na mahitaji yao na sio miradi inayoamuliwa na kampuni wawekezaji” alisema.
Aliongeza kuwa Miongozo hiyo inakwenda kutatua changamoto ya misuguano iliyokuwepo baina ya wananchi na wawekezaji kwani hapo awali miradi iliyokuwa ikitekelezwa ilijikita zaidi kwenye utashi wa mwekezaji na sio mahitaji halisi yalipo kwenye jamii husika jambo ambalo linakwenda kutatuliwa na Miongozo hii kwani wawekezaji watawajibika kutekeleza miradi hii kulingana na uhitaji uliopo.
Katika ziara hiyo, ujumbe wa PURA ulitembelea kituo kipya cha afya cha Songo Songo, bweni na maabara ya sayansi katika Shule ya Sekondari Songo Songo ambavyo vyote kwa pamoja vimejengea na kampuni ya PAET ikiwa ni baadhi ya miradi ya CSR inayoitekeleza kisiwani humo.
Ujumbe huo pia ulisikiliza wasilisho la miradi ya CSR inayotekelezwa na TPDC ambayo ni pamoja na kutoa huduma za maji na umeme bure kwa wananchi wa kisiwa hicho huku jitihada za kuwaletea kivuko cha uhakika wananchi hao zikiwa zinaendelea.
Akizungumza wakati wa ziara hiyo, Mjiolojia Desmond Risso aliyemwakilisha Mkurugenzi Mkuu wa PURA, amesema wamefarijika kuona juhudi zinazofanywa na wawekezaji katika eneo hilo huku akifurahishwa na namna ambavyo Diwani amewataka wananchi kutumia miradi hiyo kwa namna ambayo imekusudiwa.
Akigusia kuhusu uanzishwaji wa Miongozo hiyo ya utekelezaji wa CSR, Risso alisema imelenga kuhakikisha jamii inayozunguka miradi hiyo zinahusishwa katika kuamua miradi inayotakiwa kupewa kipaumbele badala ya kuwa na miradi isiyokuwa mahitaji halisi ya wananchi
"Nitoe wito kwa wana Songo Songo, pale ambapo miongozo hii itakuwa tayari kuwe na utayari wa watu kujitokeza na kushiriki katika kuibua mahitaji halisi yaliyopo kwenye eneo hili, ili kwamba miradi inayotekelezwa itatue kero zilizopo na hivyo kuboresha maisha ya wakazi wa kisiwa hiki," aliongeza Risso.
Mjiolojia Desmond Risso akizungumza jambo na Diwani wa Kata ya Songo Songo Mhe. Hassan Swalehe Yusuph alipomwakilisha Mkurugenzi Mkuu wa PURA katika ziara ya hivi karibuni ya wataalamu wa PURA na wadau wa habari kutembelea Miradi ya Uwajibikaji kwa Jamii (CSR) inayotekelezwa kisiwani Songosongo.
Meneja Operesheni wa Kampuni ya PanAfrican Energy Tanzania (PAET) Bw. Peter Sololo akitoa maelezo ya kiufundi kwa wataalamu wa PURA na wanahabari wakati wa ziara yao katika mitambo ya uzalishaji na uchakataji gesi asilia wa kampuni hiyo kisiwani Songo Songo, iliyofanyika hivi karibuni.
Mjiolojia Desmond Risso akizungumza na Meneja Kiwanda cha uchakataji gesi asilia cha GASCO kisiwani Songo Songo Mha. James Mwaipasi wakati wa ziara ya wataalamu wa PURA na wadau wa habari kutembelea Miradi ya Uwajibikaji kwa Jamii (CSR) kisiwani humo hivi karibuni. Bw. Risso alimwakilisha Mkurugenzi Mkuu wa PURA katika ziara hiyo.
Meneja Operesheni wa Kampuni ya PanAfrican Energy Tanzania (PAET) Bw. Peter Sololo akizungumza na Mjiolojia wa PURA, Desmond Risso aliyemwakilisha Mkurugenzi Mkuu wakati wa ziara ya kutembelea Miradi ya Uwajibikaji kwa Jamii (CSR) inayotekelezwa kisiwani Songo Songo. Ziara hiyo ilifanyika hivi karibuni.
Wataalamu wa PURA, TPDC, PAET na wanahabari wakiwa katika picha ya pamoja wakati wa ziara ya kutembelea Miradi ya Uwajibikaji kwa Jamii (CSR) inayotekelezwa kisiwani Songo Songo iliyofanyika hivi karibuni.