Wakazi wa Mitaa ya Kigogo Fresh A na B Kata ya Pugu Wilaya ya Ilala Jijini Dar es salaam waeleza kuridhishwa na upatikanaji wa huduma ya maji katika maeneo yao kufuatia kukamilika kwa maboresho makubwa katika kituo cha kusukuma maji Kibamba yaliyotekelezwa na Mamlaka ya Majisafi na Usafi wa Mazingira Dar es Salaam (DAWASA).
Ndugu Asha Ally, Mkazi wa Kigogo Fresh A, ameeleza kuwa, awali walipata maji kwa msukumo mdogo sana sambamba na mgao mkubwa ambapo walikuwa wakipata maji mara moja au mbili kwa wiki tofauti na hali ilivyo sasa.
"Tangu jana usiku tumepata maji mengi na msukumo umeongezeka, hali hii inaridhisha sana, tunashukuru kwa maboresho yaliyotekelezwa na DAWASA, tunategemea kupata huduma ya maji kwa siku tatu hadi nne ndani ya wiki jambo ambalo litafanya shughuli zetu nyingi kusogea," ameeleza Ndugu Asha.
Nae Mjumbe wa Mtaa wa Kigogo Fresh A, Ndugu Hussein Chacha ameishukuru DAWASA kwa maboresho wanayoendelea kufanya ili wananchi wapate huduma bora na yakutosheleza kwa wakati wote.
"Kilio chetu kikubwa wananchi ni huduma bora za majisafi, tunaipongeza DAWASA kwakua wanatatua changamoto iliyokuwepo kwa vitendo na mabadiliko yanaonekana, niwaombe wasichoke kutoa huduma hii bora kwa wananchi," ameeleza Ndugu Chacha.
Matokeo haya chanya ya huduma ya maji ni jitihada zinazofanywa na DAWASA kwa kuboresha kituo cha kusukuma maji Kibamba, zoezi lililohusisha ufungaji wa pampu mpya yenye uwezo wa kusukuma maji lita laki 2 kwa saa na ufungaji wa transfoma kubwa yenye uwezo wa kutoa umeme wa kilovoti 1000 kutoka kilovoti 500 za awali.
Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia langolahabari@gmail.com au WhatsaApp: +255 621 896 990
Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia langolahabari@gmail.com au WhatsaApp: + 255 621 615 613 au +255 621 896 990