Na Mwandishi Wetu, Dodoma
MAKAMU wa Rais Dk.Philip Mpango ameeleza kwa kina kuhusu hatua zinazopaswa kuchukuliwa katika kuhamasisha nishati safi ya kupikia huku akitumia nafasi hiyo kuipongeza Kampuni ya Oryx Gas kwa kuunga mkono kampeni hiyo kwa kugawa mitungi ya gesi kwa makundi mbalimbali yakiwemo ya wanawake.
Aidha ametoa mwito sekta binafsi kuunga mkono na kuchangia katika kampeni ya kuondokana na matumizi ya nishati chafu na kwamba mkakati wa Serikali ni kuhakikisha nishati hiyo inapatikana kwa urahisi na gharama nafuu.
Akizungumza jijini Dodoma alipokuwa akifungua Kongamano la Wanawake la kugawa mitaji na vitendea kazi vya nishati safi ya kupikia yakiwemo majiko ya gesi ya Oryx,Dk.Mpango ameeleza juhudi za Serikali kwa kushirikiana na wadau katika kuhamasisha nishati safi ya kupikia.
Amesisitiza sekta binafsi zinaweza kusaidia kuwekeza katika utafiti, ubunifu na uzalishaji wa nishati safi na nafuu ya kupikia.“Naiomba sekta sekta binafsi kutumia mifuko ya wajibu wenu kwa jamii kuwezesha kaya zinazowazunguka kupata nishati safi ya kupikia mijini na vijijini.
“Sekta binafsi pia inaweza kushirikiana na watu binafsi kueneza matumizi ya nishati safi ya kupikia.Kwa mfano kampuni ya Oryx Gas inafanya kazi na taasisi ya Dorris Mollel Foundation kusaidia akina mama katika maeneo mbalimbali ya nchi yetu.”
Kwa upand wake Mkurugenzi wa Oryx Gas Tanzania Benoit Araman amesema kampuni hiyo imeweka mkakati maalum wa kukuza matumizi ya nishati safi ya kupikia na mpaka sasa wameshatoa mitungi ya gesi na majiko yake zaidi ya 24000 yenye thamani ya Sh.bilioni 2 kwa makundi mbalimbali ya wanawake.
“Kwa zaidi ya miaka 15, upatikanaji wa suluhisho la kupikia kwa nishati safi umekuwa ukijadiliwa na kupangwa, lakini sasa imekuwa mada ya muhimu, chini ya uongozi wa Rais Dk. Samia Suluhu Hassan na serikali yake.
Amesema kuwa takwimu zinaonesha nchini Tanzania, wananchi 33,000 wanapoteza maisha kila mwaka kwa kuvuta moshi na chembechembe zinazotokana na mkaa na kuni, hivyo kupika kwa gesi ya Oryx itatatua changamoto hiyo.
Pia amesema kupika kwa gesi kunasaidia katika kulinda mazingira kwani huzuia ukataji miti, hivyo husaidia kulinda mazingira
Kuhusu hali za maisha amesema kupika kwa kutumia gesi ya Oryx huzuia wanawake kutumia saa nyingi kwa ajili ya kukusanya kuni kutoka msituni huku pia akielezea namna ambavyo gesi inavyosaidia wanawake kukabiliwa na hatari katika misitu ya wanyamapori pamoja na kukutana na majanga mengine.
“Kupika kwa kutumia gesi ya Oryx ni kupika kwa haraka na kwa ufanisi kwa hivyo kutawaruhusu wanawake kuwa na muda zaidi kusoma, kufanya kazi za jamii na maendeleo ya kibinafsi.
“Kupika kwa kutumia gesi ya Oryx ni kupika kwa haraka na kwa ufanisi zaidi; kwa hiyo, wanawake wataanda chakula kwa wakati na wanaume hawatalalamika juu ya kuchelewa kwa chakula kinachosababisha mizogo.
“Timu nzima ya Oryx Gas Tanzania inajivunia kufanya kazi kila siku kusaidia mpango wa upatikanaji wa upishi kwa nishati safi kwa wakazi wa Tanzania. Kwa hivyo, Oryx Gas itaendelea kufanya kazi kwa bidii ili kutekeleza maono ya Rais kuhusu upatikanaji wa nishati safi,”amesema Benoit.